Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

FCC YAZINDUA KAMPENI YA UTOAJI ELIMU KWA UMMA KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA MLAJI DUNIANI



Tume ya Ushindani (FCC) imeanza rasmi maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki ya Mlaji Duniani kwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya utoaji elimu kwa umma.

Kupitia kampeni hiyo, walaji na wafanyabiashara watapatiwa mafunzo yanayolenga kuwajengea uelewa kuhusu haki, wajibu na misingi ya ushindani wa haki katika soko.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema dhamira kuu ni kumwezesha mlaji kuwa na uelewa mpana kabla ya kufanya maamuzi ya kununua bidhaa au kupata huduma.

Ameeleza kuwa mlaji anapaswa kutambua namna ya kuchukua hatua pale anapokumbana na bidhaa hafifu au huduma zisizoendana na matakwa ya kisheria.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume hiyo, kilele cha maadhimisho kitafanyika Machi 31, 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, huku Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.



Katika kuadhimisha siku hiyo, FCC imepanga kutumia redio, televisheni na mitandao ya kijamii kusambaza ujumbe wa elimu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.



Sambamba na hilo, kliniki za walaji zitafanyika katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Musoma, Njombe na Tanga kwa ajili ya kusikiliza na kutatua malalamiko ya wananchi.



Aidha, semina kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya ujenzi pamoja na matumizi ya magari ya matangazo zitatekelezwa mwezi Machi, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza na kuwasilisha changamoto zao kwa hatua stahiki.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com