Tanzania imepiga hatua kubwa katika ramani ya dunia kwa kuweka Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024-2034, ukiwa ni mpango jumuishi unaolenga kukabiliana na uharibifu wa mazingira pamoja na athari mbaya za kiafya, kiuchumi na kijamii.
Maono haya ya kitaifa yalianza kupata mwelekeo madhubuti mnamo Novemba 2022, wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipoelekeza kuandaliwa kwa mkakati utakaohakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanahamia kwenye nishati safi ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo.
Katika kuunga mkono maono hayo ya Rais, Shirika la Maendeleo ya Kijamii la REDESO, kwa ufadhili wa Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa (IDRC), limezindua mradi kabambe unaolenga kuwajengea uwezo wanawake na vijana 1,600 nchini.
Mradi huu unatekelezwa kupitia vyuo sita vya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika mikoa ya Dodoma, Mwanza, Singida, Dar es Salaam na Pwani.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa REDESO, Abeid Kasaizi, anabainisha kuwa mradi huo umejikita katika kuandaa mitaala ya kozi fupi na ndefu itakayowezesha vituo vya mafunzo kufundisha teknolojia za kisasa zikiwemo za majiko banifu, mifumo ya sola, na usafiri wa umeme.
Umuhimu wa mradi huu unajidhihirisha katika namna unavyoziba pengo la ujuzi ambalo limekuwa likiwazuia wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nishati jadidifu.
Kwa mujibu wa Kasaizi, lengo si kutoa ujuzi wa kiufundi pekee, bali ni kuchochea ari ya ujasiriamali ili wahitimu waweze kuanzisha biashara zao ndani ya mnyororo wa thamani wa nishati safi.
Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa mabadiliko ya teknolojia hayaishii mijini pekee, bali yanafika hadi vijijini ambako mahitaji ya majiko banifu ni makubwa kutokana na utegemezi wa mkaa na kuni unaoendelea kuangamiza misitu yetu.
Upande wa VETA, Mkurugenzi wa Kanda ya Dar es Salaam, Wilhard Soko, anasisitiza kuwa mafunzo hayo yamejengwa juu ya msingi wa utafiti wa soko la ajira uliosaidia kubaini ujuzi halisi unaohitajika kwa sasa.
Kupitia mitaala mipya inayozingatia umahiri, vijana wa Tanzania wanatayarishwa kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa umahiri mkubwa si tu ndani ya nchi, bali hata katika soko la Afrika Mashariki na kwingineko duniani.
Ushirikiano huu kati ya VETA na REDESO unaimarisha taasisi za mafunzo kuwa chimbuko la wataalamu watakaosimamia ufungaji, matengenezo, na miundombinu ya nishati jadidifu nchini.
Social Plugin