Katibu Tawala Mkoani Shinyanga CP. Salum Hamduni akizindua rasmi Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa mazao ya choroko na dengu katika Wilaya ya Kishapu, mkoani humo Machi 3,2026
Na Sumai Salum-Kishapu
Katibu Tawala Mkoani Shinyanga CP. Salum Hamduni amezindua rasmi Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa mazao ya choroko na dengu katika Wilaya ya Kishapu, mkoani humo, hatua inayolenga kuimarisha kilimo cha kibiashara, kuongeza kipato cha wakulima na kukuza mapato ya Halmashauri.
Uzinduzi huo umefanyika mapema leo Machi 3,2026 ambapo amesisitiza kuwa mfumo huo ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wakulima kupata masoko yenye uhakika na bei shindani. Amesema stakabadhi ghalani itasaidia kupunguza changamoto ya udalali, kuimarisha ubora wa mazao na kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa kutumia mazao yao kama dhamana.
"Kama bei ya choroko kwa kilo moja ni 1500 hivyo tunaamini mkulima wa zao hili atapata faida zaidi kulipo mkulima wa zao la mpunga sasa tuwasaidie wananchi wetu ili waachane na kilimo cha mazoea kwani uhitaji wa choroko ni mkubwa kuliko uzalishaji kwa sasa" ameongeza Hamduni
Hata hivyo Hamduni amemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo kuendelea kusimamia kwa nguvu zaidi usimamizi wa wakulima kwa kuwapa elimu ya kufuata na kutumia kanuni bora na za kisasa za kilimo ili wasitumie nguvu nyingi na kupata mazao machache na yasiyo bora.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, amepokea maelekezo hayo na ameagiza wataalamu wa kilimo, biashara na ushirika kuhakikisha maelekezo yote ya kitaalamu yanatekelezwa ipasavyo ili mfumo wa stakabadhi ghalani uwe na tija kwa wakulima. Amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu endelevu kwa wakulima kuhusu ubora wa mazao, uhifadhi sahihi, na kufuata viwango vinavyotakiwa sokoni.
Aidha, amesema atasimamia kwa karibu taratibu za upokeaji na uhifadhi wa mazao ghalani ili kuzingatia ubora na uwazi, pamoja na kuandaa takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga uzalishaji na masoko kwa misimu ijayo.
Johnson ameongeza kuwa Halmashauri itahakikisha inasimamia kikamilifu utekelezaji wa mfumo huo, sambamba na kuanzisha mashamba darasa katika bajeti ijayo ya 2026/2027 ili kuhamasisha kilimo cha kibiashara chenye tija.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Viwanda, Biashara na uwekezaji mkoani humo Margareth Warioba amesema uzinduzi wa mfumo huo wa Stakabadhi ghalani chini ya usimamizi wa mamlaka ya udhubiti wa stakabadhi za ghala ni hatua muhimu katika kuwawezesha wakulima kupata bei bora, mitaji nafuu nakuchochea ukuaji wa viwanda na biashara nchini.
Meneja wa Kishapu Food Processor Edward Emmanuel Mwigulu, amesema ghala lao lina uwezo wa kuhifadhi tani 500 za mazao, ambapo hadi sasa wamekusanya takribani tani 200 za choroko. Ameeleza kuwa bei ya choroko kwa sasa ni shilingi 1,500 kwa kilo, hali inayowapa wakulima fursa ya kunufaika na soko la ushindani kupitia mfumo huo.
Imeelezwa kuwa msimu wa kilimo wa mwaka huu ni mkubwa zaidi kuliko mwaka jana, jambo linaloashiria kuongezeka kwa uzalishaji na matarajio ya mapato zaidi kwa wakulima na Halmashauri kwa ujumla.
Uzinduzi wa mfumo wa stakabadhi ghalani unatajwa kuwa chachu ya mageuzi ya sekta ya kilimo katika Wilaya ya Kishapu, ukiwawezesha wakulima kulima kwa tija, kuongeza thamani ya mazao yao na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda.
Social Plugin