MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira, ameweka jiwe la msingi ujenzi wa ofisi mpya za Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Bunda mkoani Mara, ambapo amesema tukio la kuchomwa kwa nyumba yake na ofisi ya chama OKTOBA 29,2025 halitamrudisha nyuma, bali limempa nguvu mpya ya kuhamasisha ujenzi upya kwa mshikamano wa wanachama.
Akizindua ujenzi huo na kuweka jiwe la msingi katika ofisi hiyo Leo Machi 27,2026 Wilayani Bunda, Makamu huyo Mwenyekiti, amesema aliamua kutumia akili, ushawishi na mtandao wake mpana wa marafiki kuanzisha wazo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kujenga upya ofisi ya chama hicho.
Amesisitiza kuwa jengo hilo si mali binafsi, bali ni mali ya wanachama wote wa CCM, jambo lililompa uhalali wa kuomba mchango kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya eneo hilo.
"Mwitikio ulikuwa mkubwa, ambapo marafiki na wadau kutoka sehemu mbalimbali waliunga mkono juhudi hizo, hatua iliyowezesha kuanza kwa ujenzi ndani ya muda mfupi",amesema.
Aidha, Amesema wao walidhani wanaichoma CCM kumbe CCM huwezi kuichoma na wala haichomeki na sisi tuliwambia Asanteni sana tukawambia tutajenga nzuri kuliko mliyochoma.
"Kwakuwa walichoma nyumba yangu na ofisi ya CCM na mimi ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa hiyo walikuwa hawagombani na Mimi bali walikuwa wanagombana na CCM nikaanzisha wazo la ujenzi wa ofisi wakati najenga nyumba yangu na ujenzi wa ofisi ya CCM inajengwa",amesema.
“Siwezi kuchangisha kwa ajili ya nyumba yangu binafsi, lakini ofisi ya chama ni ya wanachama wote—hapa lazima tushirikiane,” amesema Wasira kwa msisitizo.
Kadhalika, amesema kuwa dhamira yake ni kuona ofisi hiyo inajengwa upya na kuwa ishara ya mshikamano, uthabiti na imani ya wanachama katika chama chao, hata wanapokumbana na changamoto kubwa.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa MNEC wa mkoa wa Mwanza Jamal Abdul Babu amempongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Wasira kwa uamuzi huo wa kishujaa ambapo amesema ameonesha mfano wa uongozi wa vitendo na kuamsha matumaini mapya kwa wanachama.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bunda Ndug. Mayaya Abraham Magesse amesema juhudi hizo alozozifanya Makamu Mwenyekiti wa CCM Wasira zimeacha alama kubwa katika eneo hilo na zimeongeza ari ya wanachama kushiriki kikamilifu katika ujenzi.
Uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa jengo la ofisi za CCM Wilaya ya Bunda ni kutokana na ofisi hiyo kuchomwa Moto katika vurugu za Oktoba 29, 2025.













Social Plugin