Mbunge wa Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akiwasilisha changamoto za huduma za afya mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara.Na Mapuli Kitina Misalaba
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya katika jimbo hilo jipya kutokana na uhaba wa vituo vya afya, zahanati chache pamoja na maboma mengi ya zahanati ambayo hayajakamilishwa.
Mhe. Azza amesema hayo
leo Februari Mosi, 2026, wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongella, alipotembelea Kituo cha Afya cha Tinde
mkoani Shinyanga kusikiliza kero za wananchi na kujionea hali ya utoaji huduma.
Amesema Jimbo la Itwangi
lina vituo vya afya viwili pekee ambavyo ni Kituo cha Afya cha Tinde na Kituo
cha Afya cha Samuye, huku likiwa na vijiji 58 lakini zahanati 23 tu ndizo
zinazofanya kazi, wakati maboma 26 ya zahanati bado hayajakamilishwa.
Ameeleza kuwa anatamani
kila kata iwe na kituo cha afya, lakini utekelezaji wake unafanyika kwa awamu
kutokana na uwezo wa rasilimali zilizopo, huku akibainisha kuwa tayari
amewasiliana na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ambaye amezichukua
changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi.
Kwa upande wake, Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, amesema atawasiliana na Waziri wa Afya
pamoja na Waziri wa TAMISEMI ili kuhakikisha miundombinu ya Kituo cha Afya cha
Tinde inaboreshwa, hatua itakayosaidia kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi wa
eneo hilo.
Mongella pia amepongeza
jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha huduma za afya
nchini, akisisitiza kuwa CCM itaendelea kusimamia utekelezaji wa ahadi zake kwa
wananchi.
Baadhi ya wakazi wa Jimbo la Itwangi akiwemo Sabina Mwang’onda, Amina Sanga, Mwajuma Masanja na Masanja Charles, wamekiri kuwepo kwa changamoto za huduma za afya kama zilivyobainishwa na mbunge wao, huku wakiomba Serikali kuzifanyia kazi kwa haraka ili kuboresha maisha ya wananchi wa jimbo hilo.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho
ya Miaka 49 ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo
inasema “TUMECHAGUA
UMOJA NA AMANI KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU.”
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, akizungumza na wananchi baada ya kukagua Kituo cha Afya cha Tinde Jimbo la Itwangi.
Mganga mfawidhi wa Kituo cha Afya Tinde, Evas Monis, akieleza kuwa upatikanaji wa dawa katika kituo hicho umefikia asilimia 95.
Viongozi wakitembelea Kituo cha Afya cha Tinde, Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga, kwa lengo la kukagua huduma na kusikiliza kero za wananchi.
Viongozi wakitembelea Kituo cha Afya cha Tinde, Jimbo la Itwangi mkoani Shinyanga, kwa lengo la kukagua huduma na kusikiliza kero za wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella,
akikabidhi zawadi mbalimbali kwa wagonjwa katika kituo cha Afya Tinde jimbo la
Itwangi.

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe.
Azza Hillal Hamad, akikabidhi zawadi kwa wagonjwa mbalimbali
katika kituo cha Afya Tinde.

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe.
Azza Hillal Hamad, akikabidhi zawadi kwa wagonjwa mbalimbali
katika kituo cha Afya Tinde.

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe.
Azza Hillal Hamad, akikabidhi zawadi kwa wagonjwa mbalimbali
katika kituo cha Afya Tinde.







Social Plugin