Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU : SERIKALI IMEONGEZA NGUVU TAKUKURU KULINDA RASILIMALI ZA TAIFA

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa hatua madhubuti ikiwemo kuongeza rasilimali watu, bajeti, miundombinu na kufanya marekebisho ya kisheria, hatua zilizoongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya rushwa na kuifanya Tanzania kuwa mfano wa utawala bora barani Afrika.

Akizungumza leo Jumatatu, Januari 26, 2026, mkoani Morogoro alipomwakilisha Rais Samia katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika katika Ukumbi wa Cate Convention Centre, Waziri Mkuu amesema juhudi hizo zimewezesha TAKUKURU kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 60.2 ambazo zimeelekezwa kwenye huduma muhimu za jamii zikiwemo afya, elimu, maji, umeme na miundombinu.

Dkt. Nchemba amebainisha kuwa mifumo imara ya udhibiti wa rushwa na usimamizi wa rasilimali iliyojengwa na Serikali imeifanya Tanzania kusimama imara hata mbele ya changamoto za kiutawala zinazozikumba nchi nyingine, na hivyo kuwa kielelezo kwa mataifa mengi ya Afrika katika masuala ya uwajibikaji na uadilifu.

“Wapo watu na hata mataifa yanayoikosoa Tanzania mitandaoni, lakini ukweli ni kwamba wengi wao wanahangaika kwa sababu wameshindwa kufikia kiwango cha mifumo ya udhibiti tuliyonayo hapa nchini,” amesema Dkt. Nchemba.
Katika kuwasilisha ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Rais hapendi wala havumilii rushwa, ubadhirifu wa mali za umma au uzembe kazini, na kwamba dhamira yake ya kulinda utu wa mwananchi na kuleta maendeleo ya kweli inategemea kwa kiasi kikubwa uadilifu wa taasisi za udhibiti, hususan TAKUKURU.

Ameeleza kuwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, TAKUKURU iliendesha kesi 489 mahakamani, ambapo Jamhuri ilishinda kwa asilimia 68.8 ya kesi zilizotolewa uamuzi, jambo linaloonesha ubora wa uchunguzi na ushirikiano mzuri kati ya TAKUKURU na Mahakama ya Tanzania.

Katika kipindi hicho pia, TAKUKURU ilifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 619 yenye thamani ya Shilingi bilioni 553.45 na kufanikiwa kuokoa Shilingi milioni 173.5 zilizokuwa hatarini kupotea kutokana na mianya ya rushwa.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa rushwa inadhalilisha utu wa binadamu na inazorotesha utoaji wa huduma za jamii, hivyo akazitaka taasisi za Serikali kubaini na kuziba mianya ya rushwa hususan katika maeneo ya manunuzi ya umma, utekelezaji wa miradi na usimamizi wa mikataba, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya bajeti ya Serikali hupitia katika maeneo hayo.

Aidha, amewahimiza Watanzania kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, akisisitiza kuwa Serikali inalinda usiri na usalama wa watoa taarifa, sambamba na kuendelea kushirikisha sekta binafsi, wadau wa maendeleo, vijana na wanawake katika mapambano dhidi ya rushwa.

Dkt. Nchemba pia amesisitiza kuwa Serikali iko tayari kufanya marekebisho ya kisheria na kiutawala pale itakapobainika kuna vikwazo vinavyoathiri utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU, na kuagiza ushirikiano wa karibu kati ya TAKUKURU na Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma ili kuimarisha uadilifu katika utumishi wa umma.

Akihusisha mapambano dhidi ya rushwa na mwelekeo wa Taifa, Waziri Mkuu amesema jitihada hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025–2030, ambazo zinatambua mapambano dhidi ya rushwa kama nguzo muhimu ya demokrasia, utawala bora na ustawi wa wananchi.

Waziri Mkuu amehitimisha hotuba yake kwa kutoa wito kwa viongozi wa TAKUKURU kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanakuwa chachu ya kuongeza bidii zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao, huku akisisitiza kaulimbiu ya mkutano:

“Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com