Wanafunzi wa shule ya sekondari Rwepas, wilayani Kahama mkoani Shinyanga, wameshauriwa kuendelea kupenda na kusoma masomo ya sayansi kutokana na nafasi yake kubwa katika kujiajiri na kuajiriwa mara baada ya kuhitimu masomo yao.
Ushauri
huo umetolewa na mgeni rasmi, Ofisa Mkaguzi na Mdhibiti Ubora wa Shule Manispaa
ya Kahama, Lazaro Malili, katika mahafali ya 19 ya kidato cha
nne yaliyofanyika shuleni hapo. Malili amesema bado kuna changamoto ya baadhi
ya wanafunzi kuogopa kusoma masomo ya sayansi licha ya fursa nyingi zilizomo
ndani yake.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Malili amesema serikali imeweka mitaala miwili ya elimu mkondo
wa amali na mkondo wa ujumla ambayo humwezesha mwanafunzi kusoma kile
anachokipenda, huku akibainisha kuwa masomo ya sayansi yana mchango mkubwa
katika maisha ya kila siku. “Masomo ya sayansi yamebeba fani nyingi ikiwemo
uhandisi, udaktari, kilimo cha mifugo, kilimo cha mazao na utunzaji wa
mazingira. Mwanafunzi akiyapenda na kuyamudu vizuri, anaweza kujiajiri bila kusubiri
kuajiriwa,” amesema Malili.
Kwa upande wake, Mhandisi Happines Malila kutoka Chuo cha Madini Shinyanga,
amewatia moyo wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi bila woga, akisema
dhana kwamba ni masomo ya wavulana pekee si sahihi. “Nilipambana, nikavumilia
changamoto na sasa naona matunda ya juhudi zangu. Hivyo basi, nawaomba msisite
kuyapenda masomo haya,” amesema.
Aidha, wazazi waliokuwa sehemu ya mahafali hayo, akiwemo Monica Julius na Biles Ntangalo, wamewashauri wanafunzi wahitimu kuepuka makundi mabaya mitaani na badala yake wajitunze wakisubiri matokeo ya mitihani yao.
Nao baadhi ya
wahitimu, Agnes Patrick na Alphan Majid,
walisema wamechagua masomo ya sayansi kwa hiari kwa kuwa yanaendana na vipaji
vyao na yatawasaidia hata katika maisha ya nyumbani.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Frank Samweli, amesema kwa sasa
shule ina jumla ya wanafunzi zaidi ya 500 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha
nne, ambapo wahitimu wa mwaka huu ni 73 wasichana 40 na wavulana 33 na
matarajio ni wote kufaulu na kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo.

Social Plugin