Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HUDUMA YA MAJI KIJIJI CHA NYASAMBA - KISHAPU YAREJEA! WANANCHI WAPONGEZA HATUA ZA HARAKA


Wakazi wa Kijiji cha Nyasamba, Wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, waliokuwa wakikabiliwa na ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kufutia kuharibika kwa pampu ya kisima kirefu hatimaye imetatuliwa baada ya Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufanikisha matengenezo yake.

Tatizo hilo la maji lililodumu kwa siku kadhaa lilisababisha zaidi ya kaya 800 za kijiji hicho kukosa huduma ya maji safi, na kuwalazimu wakazi wa eneo hilo kutafuta maji katika mabwawa na vyanzo visivyo salama, hali iliyowaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya tumbo na ya mlipuko.

Akizungumza kwa furaha baada ya kurejea kwa huduma ya maji, Anatolia William na Leah Samwel, wakazi wa Nyasamba, wamesema walipata shida kubwa wakati wa hitilafu hiyo, hasa wanawake na watoto waliolazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji yasiyo salama.

“Tulilazimika kwenda kwenye mabwawa ambayo tunajua si salama, lakini hatukuwa na njia nyingine. Tunamshukuru Mungu na RUWASA kwa kuturejeshea huduma ya maji,” amesema Leah Samwel.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyasamba, Martin Kafumu, amethibitisha kuwa tatizo hilo limepatiwa suluhisho na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya maji kwa manufaa ya jamii yote.

“Changamoto ilikuwa kubwa, lakini sasa wananchi wetu wamepata nafuu. Tunawashukuru RUWASA kwa hatua ya haraka,” amesema Kafumu.

Kwa upande wake, msimamizi wa kituo cha kuchotea maji kinachosimamiwa na Jumuiya ya Watumia Maji (CBWSO), Christina Koyo, ameeleza jinsi huduma hiyo ilivyokatika ghafla, na kuwapa wananchi wakati mgumu, lakini kwa sasa huduma imerejea kwa ufanisi mkubwa.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Dickson Kamazima, ameeleza kuwa hitilafu hiyo ilitokana na uchakavu wa pampu, lakini mafundi walichukua hatua za haraka kuhakikisha huduma inarejea mapema.

“Tunawahimiza wananchi waache kutumia maji ya mabwawa na madimbwi ambayo si salama kiafya. RUWASA itaendelea kuhakikisha huduma ya maji safi inapatikana kwa wote,” amesema Kamazima.

Kurejea kwa huduma ya maji safi katika Kijiji cha Nyasamba ni ushahidi wa kazi inayoendelea kufanywa na serikali kupitia RUWASA kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma ya maji safi, salama na ya uhakika.



























Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com