Aagiza TANROAD, TARURA, AUWSA, TANESCO na TTCL kujenga miundombinu muhimu haraka
Ampongeza Rais Samia kwa kutoa Sh Bilioni 340 kujenga uwanja huo wa kisasa
Na Woinde Shizza , Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Gabriel Makalla, leo Ijumaa Septemba 05, 2025, ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu utakaotumika katika mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027). Uwanja huo unajengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 340 katika Kata ya Olmot, Jijini Arusha.
Ukaguzi huo ulitanguliwa na kikao kazi kilichowakutanisha wakuu wa idara na mamlaka husika za maji, nishati, barabara na mawasiliano. Katika kikao hicho, kiliundwa Kikosi kazi cha wataalamu wa sekta hizo kitakachosimamia uwekaji wa miundombinu yote muhimu chini ya uratibu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, RC Makalla alisema Kama Mkoa wa Arusha tunajivunia utalii. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa kupitia Royal Tour na sasa anatuletea utalii wa michezo (sport tourism). Uwanja huu utaleta mzunguko mkubwa wa pesa, kuchochea biashara, na kuinua uchumi wa wananchi wetu.
alisema wanamhakikishia Rais kwamba watasimamia ujenzi huo mpaka ukamilike Julai 2026 kama mkandarasi alivyoahidi
Makalla alisisitiza kuwa uwanja huo utakuwa wa kisasa na wa kimataifa, ukiwa na hadhi ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Pia alisema kuwa maamuzi ya Rais Samia ya kufadhili mradi huu kupitia mapato ya serikali ni ishara ya kuipa heshima Tanzania na kuleta fursa kubwa za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Makalla aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na mkandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, huku akiagiza mamlaka husika kuharakisha huduma za barabara, maji, nishati na mawasiliano ili miundombinu ikamilike sambamba na uwanja huo.
mwakilishi wa mkandarasi kutoka kampuni ya China Railway Construction, Mhandisi Denice Benito Mtemi, akiongea na waandishi
Kwa upande wake, mwakilishi wa mkandarasi kutoka kampuni ya China Railway Construction, Mhandisi Denice Benito Mtemi, alisema ujenzi umefikia asilimia 60. Alifafanua kuwa uwanja huo utakuwa na nyasi asilia, vyumba vinne vya kubadilishia nguo, uwanja wa mazoezi, na miundombinu mingine yote kulingana na viwango vya kimataifa.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa fedha kwa wakati, jambo lililowezesha kazi kuendelea bila vikwazo. Tunawahakikishia Watanzania kwamba uwanja huu utakamilika kwa ubora unaostahili, na utafungua fursa nyingi za uwekezaji na ajira kwa wananchi, hasa walioko jirani na eneo la mradi,” alisema Mtemi.





Social Plugin