Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIVUNGE, SABAYA, LUKUMAY NA WASIRA WATINGISHA ARUMERU MAGHARIBI KWA KISHINDO CHA KAMPENI ZA CCM


Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Martha Kivunge akiongea Katika mkutano huo

Na Woinde Shizza Arusha 

Uzinduzi wa kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Arumeru Magharibi umeendelea kushika kasi na nguvu kubwa za kisiasa baada ya viongozi wa CCM kujitokeza kwa wingi kuhamasisha wananchi kuendelea kukipigia kura chama hicho kwa kishindo kuelekea uchaguzi mkuu ujao.



Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha, Martha Kivunge, aliwataka wananchi wa Arumeru Magharibi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuhakikisha ushindi wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wote wa CCM kuanzia wabunge hadi madiwani.



“Wananchi wa Arumeru Magharibi, kura zenu ndizo silaha zetu za maendeleo ,tukimpa kura Rais wetu Mama Samia, wabunge na madiwani, tuna uhakika wa kuendelea kupata huduma bora na miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Kivunge akishangiliwa na umati wa wananchi.


Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ambaye pia alikuwa mtia nia Katika Jimbo hilo, alimpongeza Rais Samia kwa mageuzi makubwa kwenye mfumo wa sheria na kupunguza msongamano wa mahabusu.


“Niliingia gerezani nikakuta zaidi ya mahabusu 2,000, lakini nilipotoka walibaki 84 tu. Huu ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia kuhakikisha haki inatendeka,” alisema Sabaya huku akishangiliwa kwa nguvu na wananchi waliokuwa wamejitokeza kwa wingi.


Naye mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Rais Samia itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo barabara, shule, hospitali, maji safi, elimu na umeme vijijini, akiwataka wananchi kuipa CCM kura zote ili kasi hiyo iendelee.


“Mama Samia amefanikisha miradi ya barabara, shule, hospitali na huduma za maji katika maeneo mengi nchini. Arumeru pia imepata miradi hii, na kazi yetu sasa ni kuhakikisha chama kinashinda ili miradi iendelee kuwanufaisha wananchi,” alisema Wasira.


Katika shamrashamra hizo,mmoja wa watia nia  wa Jimbo hilo Elias Lukumay alimhakikishia Wasira na wananchi kuwa mshikamano wa chama na nguvu za wanachama wote ndizo zitakazohakikisha ushindi wa kishindo wa Dkt. Johannes Lukumay pamoja na kura zote za Rais Samia Suluhu Hassan katika Jimbo la Arumeru Magharibi.


“Tuta hakikisha Dkt. Lukumay anashinda kwa kishindo, na vilevile kura zote za Arumeru Magharibi zinaenda kwa Mama Samia. Huu ni wakati wa mshikamano na ushindi wa CCM,” alisema kwa kujiamini.


Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, na kushuhudiwa na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwa wingi kuonyesha mshikamano wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com