Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mkoa wa Kagera umeandika historia kwa kufanikisha hatua kubwa za maendeleo katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Aprili 2025, ambapo miradi mbalimbali ya kimkakati imeleta mageuzi makubwa katika sekta za afya, elimu, huduma za maji, nishati, kilimo, biashara na miundombinu.
Akizungumza jijini Dodoma Julai 1, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa, alieleza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita na ushirikiano thabiti kati ya wananchi, viongozi na wadau mbalimbali.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ni ongezeko la vituo vya afya na hospitali. Katika kipindi hicho, hospitali za wilaya zimeongezeka kutoka tatu hadi 11, vituo vya afya kutoka 29 hadi 42 na zahanati kutoka 217 hadi 283. Huduma za kibingwa zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa zimeongeza idadi ya wagonjwa waliotibiwa ndani ya mkoa kwa asilimia 273, ikipunguza utegemezi wa rufaa kwenda mikoa mingine kama Mwanza na Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa amesema huduma hizi za kibingwa zikiwemo upasuaji wa pua, koo na masikio, mifupa na magonjwa ya ndani, zimekuwa ni sehemu ya mageuzi ya huduma za afya katika mkoa huo.
Sekta ya elimu nayo imepata mwelekeo chanya, ambapo shule mpya za awali na msingi 116, sekondari 68 na vyuo vya VETA 5 vimejengwa. Vituo vya elimu vimeongezeka kutoka 4 hadi 9, ikiwemo Chuo cha VETA cha Burugo kilichogharimu zaidi ya shilingi bilioni 20. Vyumba vya madarasa 4,709, maabara 167 na mabweni 121 vimewekwa ili kupunguza upungufu wa miundombinu.
Ufaulu wa kitaaluma umeendelea kuimarika, ambapo ufaulu wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 91 hadi 94.57, ikionyesha juhudi za Serikali kuleta mabadiliko chanya katika elimu ya vijana wa mkoa huo.
Hatua ya kihistoria ambayo imepongezwa kwa upana ni kuunganishwa kwa umeme vijiji vyote 662 vya mkoa wa Kagera, hatua ambayo ni ya kwanza katika historia ya mkoa huo.
Vitongoji 1,763 kati ya 3,665 vimeunganishwa na umeme, hali ambayo inazusha matumaini makubwa ya maendeleo endelevu ya sekta za kilimo, biashara na huduma za kijamii.
Serikali kupitia miradi mikubwa ya kuzalisha umeme wa maji (HEP) imechangia pakubwa kupatikana kwa umeme wa uhakika, tofauti na awali ambapo mkoa ulikuwa ukitegemea umeme kutoka Uganda na jenereta.
Katika miundombinu ya barabara, jumla ya shilingi bilioni 117.9 zimewekezwa katika ujenzi na ukarabati wa barabara za mkoa, ikiwemo barabara za mijini na za changarawe. Barabara zinazounganisha makao makuu ya mkoa na wilaya zimeongezeka kutoka kilomita 783.1 hadi 800.76, huku barabara za mijini zikiwa kilomita 40.87.
Madaraja makubwa matano yamejengwa katika maeneo ya Kanoni (Bukoba Mjini), Kyanyabasa, Kyetema (Bukoba Vijijini), Kamishango na Kelebe (Muleba), kusaidia kuimarisha usafiri na biashara.
Sekta ya kilimo imepata msukumo mkubwa hasa kwa zao la kahawa ambapo Serikali imepunguza tozo kutoka 17 hadi 5, na kusababisha kupanda kwa bei kutoka shilingi 1,200 hadi 4,200 kwa kilo, pamoja na kuongeza uzalishaji hadi tani 54,203.
Wananchi wamewezeshwa kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu, ikiongezeka kutoka shilingi bilioni 3.2 hadi 9.4, na kaya zaidi ya 380,000 zimenufaika na mpango wa TASAF.
Biashara rasmi zimeongezeka kwa asilimia 55 huku wawekezaji wakisajili miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 267.1 na kutoa ajira kwa zaidi ya watu 11,000.
Mkoa umefanikiwa kutekeleza miradi 28 ya kimkakati kwa kutumia fedha za mapato ya halmashauri, ikiwemo ujenzi wa masoko ya kisasa, shule za michepuo ya Kiingereza, stendi za mabasi na barabara za lami ndani ya Manispaa ya Bukoba.
Mkuu wa Mkoa amewashukuru wananchi, viongozi wa dini na wadau wote kwa ushirikiano wao, na kuahidi kuendelea kusimamia miradi kwa weledi ili kuhakikisha mafanikio haya yanadumu na kuleta manufaa kwa vizazi vijavyo.
Social Plugin