Mtia nia ubunge Jimbo la Kishapu Bonda William Nkinga(kulia) akirejesha fomu kwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga (Kushoto) Julai 1,2025 katika ofisi za Chama hicho Wilayani humo
Na Sumai Salum - Kishapu
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Bonda William Nkinga amechukua na kurejesha rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kishapu kupitia tiketi ya Chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo Julai 1, 2025 katika Ofisi za CCM Wilaya ya Kishapu, Nkinga amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa demokrasia ndani ya chama, huku akisisitiza kuwa dhamira yake kuu ni kuleta maendeleo na mabadiliko chanya kwa wananchi wa Kishapu.
“Endapo Chama changu kitanipa ridhaa ya kuiwakilisha Kishapu, natamani kuwaonesha wananchi wenzangu fursa mbalimbali ambazo chama chetu kimekusudia kuzitekeleza. Nina uzoefu wa kufanya kazi ndani ya chama na serikalini, hivyo naamini kwa ushirikiano na wananchi, tunaweza kuiletea Kishapu mabadiliko ya kweli,” amesema Nkinga.
Nkinga amebainisha kuwa, kama atapata nafasi hiyo, atahakikisha kila mwananchi anapata taarifa sahihi kuhusu masuala yanayojadiliwa na kuidhinishwa bungeni, ili waweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake na ameahidi kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kulipa kodi ili kuiwezesha serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo akisisitiza kuelimisha vijana kuhusu fursa zilizopo, hususan kupitia Mapango wa BBT “Jenga Kesho Yako” iliyoanzishwa na Wizara ya Kilimo.
“Vijana wana nafasi kubwa katika sekta ya kilimo hivyo kupitia mpango wa BBT, wanaweza kujifunza na kujikwamua kiuchumi. Kama baadhi yao hawajui kuhusu mpango huu, nitahakikisha wanapata uelewa wa kutosha ili waweze kunufaika,” ameongeza Nkinga.
Mtia nia ya Ubunge Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Bonda William Nkinga akiwa nje ya ofisi za Chama hicho Wilayani humo wakati akirejesha fomu Julai 1,2025
Social Plugin