Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

COSTECH YARIDHISHWA NA UJENZI WA MAKAO MAKUU, KUHAMIA DODOMA MACHI 2026



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo jipya litakalokuwa Makao Makuu yake jijini Dodoma, ambalo linatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa rasmi ifikapo Machi 2026.

Mwenyekiti wa COSTECH, Profesa John Kondolo, amezungumza hayo leo Julia 31,2025 Jijini hapa mara walipofanya ziara ya kukagua maelendeo ya ujenzi na kueleza kuwa maendeleo ya ujenzi huo yanakwenda sambamba na masharti ya mkataba na kwamba linaendana na viwango vinavyohitajika kwa taasisi ya kitaifa ya utafiti na ubunifu.

“Tumeshuhudia umadhubuti wa kazi na fahari ya jengo hili ambalo linatarajiwa kuwa kitovu cha sayansi na teknolojia nchini,tunaamini litatimiza malengo ya kuimarisha tafiti na uvumbuzi,” amesema Prof. Kondolo.

Profesa Kondolo pia amesema: “Tuna imani kuwa jengo hili litakuwa chachu ya mapinduzi ya kisayansi na kiteknolojia nchini, na litasaidia kukuza uchumi wa ubunifu unaochochea ajira na maendeleo.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema mradi huo unaogharimu shilingi bilioni nane za Kitanzania unalenga kuboresha miundombinu ya utafiti na kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wanasayansi na wabunifu.

“Jengo litakuwa na kumbi za bunifu, mikutano ya wanasayansi, maabara za utafiti na nafasi kwa wabunifu kupata huduma za Atamizi,tutakapo hamia Dodoma, nafasi ya Dar es Salaam itatumiwa kikamilifu kusaidia wabunifu kuendeleza miradi yao,” amesema Dkt. Nungu.

Aidha, amesema ujenzi huo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuhakikisha shughuli za kitaifa za sayansi na teknolojia zinasimamiwa kwa karibu zaidi, huku Dodoma ikipata nafasi yake kama makao makuu ya shughuli hizo.

Masanifu wa mradi huo, Benedict Martin, amebainisha kuwa usanifu wa jengo umezingatia viwango vya kimataifa, ukiwa na ofisi za kisasa, maabara zenye vifaa vya hali ya juu na mifumo ya kidigitali ya mawasiliano.

“Tumelenga kutoa jengo zuri la kisasa ambalo litakidhi mahitaji ya COSTECH kwa muda mrefu na Linaweza kuhudumia wanasayansi na wabunifu wengi,” amesema Martin.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa COSTECH, ujenzi huo ni miongoni mwa hatua muhimu za Serikali kuelekea kujenga uchumi wa kidigitali na kufikia malengo ya maendeleo endelevu

Wadau wa sekta ya sayansi na teknolojia wamepongeza hatua hiyo wakisema itasaidia kuimarisha ekosistemu ya uvumbuzi na kuifanya Tanzania kuwa kiongozi katika maendeleo ya kiteknolojia Afrika Mashariki.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza fursa za ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na taasisi za utafiti, sambamba na kuhamasisha vijana kujihusisha na ubunifu na ujasiriamali wa kiteknolojia.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com