Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini yametakiwa kuzingatia mwongozo wa Serikali katika kutoa elimu kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, ili kuhakikisha taarifa sahihi na ushiriki wa kidemokrasia unaimarishwa.
Hayo yameelezwa leo Julai 31,2025 wakati wa maandalizi ya Kongamano la Kitaifa la NGOs litakalofanyika kuanzia Septemba 11 hadi 13, 2025 jijini Dodoma, ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kongamano hilo limeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara kwa kushirikiana na mitandao ya NGOs nchini, na litakutanisha zaidi ya mashirika 1,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, amesema kongamano hilo litakuwa jukwaa la tathmini ya miaka mitano ya utekelezaji wa kazi za NGOs, likibainisha mafanikio na changamoto zao katika kuleta maendeleo ya jamii.
“Mashirika haya yamekuwa mstari wa mbele katika maendeleo ya watu, na Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wao mkubwa, hasa katika kutoa huduma moja kwa moja kwa jamii,” amesema Mdemu.
Amesisitiza kuwa kupitia jukwaa hilo, NGOs zitashiriki kutoa maoni kwa Serikali kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu na mikakati ya kitaifa kama Dira ya Maendeleo ya Taifa, sambamba na kuhakikisha elimu ya mpiga kura inatolewa kwa kufuata mwongozo rasmi wa Serikali.
Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Vickness Mayao, amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kitaifa la tathmini na maboresho ya kazi za NGOs kwa lengo la kuimarisha maendeleo endelevu.
“Ingawa mashirika mengi hufanya kazi kupitia mitandao au ngazi za ndani, mchango wao katika jamii unaonekana wazi. Serikali imeonyesha dhamira ya kweli kwa kuyashirikisha kwenye maamuzi makubwa ya kitaifa, ikiwemo maandalizi ya Dira ya Maendeleo,” amesema Mayao.
Ameongeza kuwa mashirika yamekuwa msaada mkubwa kwa Serikali kwa kutoa huduma zinazosaidia wananchi kujitegemea, na kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Taifa ya Mtandao wa NGOs (TANGO) na Afisa Mahusiano wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Iringa, Charles Lwabulala, amesema TANGO itaendelea kuwaunganisha wanachama wake ili kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zinazokwamisha ustawi wa Taifa.
“Kongamano hili litatoa nafasi kwa mashirika kueleza changamoto zao moja kwa moja mbele ya Serikali, ili kuyatafutia majibu ya pamoja kwa ajili ya ustawi wa Taifa,” amesema Lwabulala.
Mashirika yamehimizwa kutumia kongamano hili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki za kiraia na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
Hatua hii inalenga kuongeza mwamko wa wananchi kushiriki katika kuamua mustakabali wa nchi na kuhakikisha hakuna upotoshaji wa taarifa za mpiga kura.
Aidha Maandalizi ya kongamano yanaendelea vizuri, huku wadau wakitarajia matokeo chanya yatakayoimarisha zaidi ushirikiano kati ya Serikali na NGOs kwa ustawi wa Taifa.

Social Plugin