RC KIHONGOSI AZINDUA ARUSHA JOGGING AWAMU YA PILI, AONGOZA MAZOEZI YA PAMOJA



Na Woinde Shizza, Arusha

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi, ameongoza maelfu ya wakazi wa Jiji la Arusha katika mazoezi ya pamoja yaliyoambatana na uzinduzi wa awamu ya pili ya Arusha Jogging Sports Club, huku akihimiza wananchi kudumisha mshikamano, upendo na kuzingatia afya bora kupitia mazoezi.

Mazoezi hayo yaliyofanyika jana Jumamosi Julai 19, 2025, yalianzia katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kupita maeneo ya Clocktower, Metropole, Kilombero, Arusha Technical, Mianzini, Sanawari, Hospitali ya Mount Meru na kumalizikia tena ofisini hapo.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Kihongosi alisema serikali ya Mkoa wa Arusha imejipanga kuanzisha utaratibu wa kufanya mazoezi hayo kila Jumamosi, lengo likiwa ni kuimarisha afya za wananchi, kukuza mshikamano na kujenga jamii yenye tija.


"Mazoezi haya si kwa ajili ya mwili tu bali yanasaidia kuimarisha afya ya akili, kuchochea uzalendo na mshikamano miongoni mwetu, Tutakuwa tunakutana kila Jumamosi kwa ajili ya afya ya Arusha," alisema Kihongosi.



Mkuu huyo wa mkoa aliwataka watumishi wa umma, mashirika ya binafsi na klabu mbalimbali za mbio kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kampeni hiyo mpya ya kiafya.

Mazoezi hayo pia yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo, watumishi wa taasisi za serikali, mashirika binafsi, wanafunzi na wakazi wa Arusha waliojitokeza kwa wingi kushiriki matembezi na mbio hizo za kiafya huku Wananchi wakipongeza serikali

Baadhi ya wananchi w

aliohojiwa na mwandishi wetu walieleza kufurahishwa na mpango huo wa mazoezi, wakisema unasaidia kuongeza hamasa ya kujitunza kiafya.

“Tumekuwa tukisikia tu umuhimu wa mazoezi, lakini sasa tunaona mfano kwa vitendo kutoka kwa viongozi wetu. Hii ni fursa ya kipekee kwa wakazi wa Arusha,” alisema Neema Joseph, mkazi wa Sanawari.


Kwa upande wake, Alex Mollel, ambaye ni mfanyakazi wa sekta binafsi, alisema tukio hilo limemhamasisha kuanza ratiba ya mazoezi ya kila wiki kwa ajili ya afya na kupunguza msongo wa mawazo.

Mazoezi hayo yamebeba kaulimbiu ya “Mazoezi kwa Afya, Mazoezi ni Burudani”, ikiwa ni wito kwa wakazi wa Arusha kushiriki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com