Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAMIA WAJITOKEZA MAZISHI YA DIWANI WA SOLWA


Mhe. Awadh Mbarak Aboud enzi za uhai wake.

Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kuaga mwili na kushiriki mazishi ya aliyekuwa Diwani wa Kata ya Solwa, Mhe. Awadh Mbarak Aboud, aliyefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Jumamosi Julai 19, 2025.

Marehemu Awadh , ambaye pia alikuwa ameonyesha nia ya kugombea tena nafasi ya udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alifariki dunia Julai 19,2025 katika ajali iliyotokea eneo la Ibadakuli, barabara kuu ya kuelekea Shinyanga Mjini, baada ya bajaji aliyokuwa akisafiria kugongwa na basi la abiria la Kampuni ya Frester, ambapo watu wawili walipoteza maisha.

Mazishi hayo yamefanyika Julai 21, 2025, yakihudhuriwa na viongozi wa serikali, vyama vya siasa, ndugu, jamaa, marafiki na wakazi wa Kata ya Solwa waliofika kumuaga kiongozi huyo kijana na mpenda maendeleo.
Mhe. Mboni Mhita

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akitoa salamu za pole kwa niaba ya Serikali, amesema kifo cha Awadh kimeacha simanzi kubwa kwa jamii, lakini pia ni ukumbusho kwa wote kuhusu maisha na muda tulionao duniani.

“Kila mmoja kwa imani yake amuombee pumziko la amani marehemu Awadh. Tumepoteza kijana mchapakazi, mwenye ndoto za maendeleo kwa wananchi wa Solwa,” amesema Mhe. Mhita.
Mhe. Ahmed Salum

Mbunge wa Jimbo la Solwa anayemaliza muda wake, Mhe. Ahmed Salum, kwa huzuni ameeleza namna marehemu Awadh alivyokuwa na moyo wa kujitolea na kushirikiana naye bega kwa bega katika kusukuma miradi ya maendeleo ya kata hiyo.

“Alikuwa kijana mwenye moyo wa kazi, alinisumbua kwa maendeleo ya wananchi. Tutamkumbuka daima,” amesema Mhe. Salum.
Ngasa Mboje

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga,Ngasa Mboje  amesema Awadh alikuwa kiongozi mwenye kujituma, mchangiaji wa hoja makini katika vikao vya madiwani na mfuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo ya kata yake.

“Alikuwa mfano wa kuigwa miongoni mwa madiwani. Aliweka mbele maslahi ya wananchi,” amesema Mboje.

Kwa mujibu wa taarifa za familia, marehemu ameacha mke na watoto, na jamii imeombwa kuendelea kuwaombea nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com