Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIWANI WA KATA YA SOLWA AFARIKI DUNIA ... MBUNGE AHMED SALUM ATUMA SALAMU ZA POLE

 

Aliyekuwa Diwani wa Kata ya Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Awadh Mbaraka Aboudamefariki dunia Julai 19,2025 katika ajali iliyotokea eneo la Ibadakuli, barabara kuu ya kuelekea Shinyanga Mjini, baada ya bajaji aliyokuwa akisafiria kugongwa na basi la abiria la Kampuni ya Frester.

Taarifa zinaeleza kuwa marehemu alikuwa safarini kutoka eneo la Kolandoto kuelekea Shinyanga Mjini akiwa ndani ya bajaji, kabla ya kugongwa na basi la kampuni ya Frester, na kusababisha majeraha makubwa yaliyompelekea kufariki dunia pamoja na mtu mwingine.

Msiba huu mkubwa umeacha simanzi kwa familia, wananchi wa Kata ya Solwa, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na jamii nzima ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Kupitia mitandao ya kijamii, Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, ameeleza masikitiko yake makubwa kufuatia msiba huo:

"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Ndugu Awadhi Mbaraka Aboud, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Solwa, kilichotokea siku ya Jumamosi, tarehe 19 Julai 2025.. Ameacha alama kubwa katika utumishi wake kwa wananchi wa Kata ya Solwa. Tumempoteza mtu muhimu sana, aliyekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo na kutetea maslahi ya
wananchi," amesema Mhe. Ahmed Salum.

Mhe. Mbunge ameeleza kuwa kifo cha Diwani Awadhi ni pigo kubwa kwa jamii ya Solwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kwa wananchi wote waliomfahamu kama kiongozi mwadilifu, mchapakazi na mpenda maendeleo.

Mhe. Ahmed Salum ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wakazi wote wa Kata ya Solwa, akiwasihi kuwa na moyo wa subira na kuendelea kuenzi mema ya marehemu.

Malunde Media tunatoa pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Solwa, viongozi wenzake, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

soma pia

MAMIA WAJITOKEZA MAZISHI YA DIWANI WA SOLWA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com