Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

EMMANUEL NTOBI ASEMA BASI NA CHADEMA, AINGIA ACT WAZALENDO KWA KISHINDO

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi, amejiunga rasmi na Chama cha ACT Wazalendo, ambapo amepokelewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu.

Akizungumza katika hafla fupi ya kuwapokea wanachama wapya, Ado Shaibu amesema chama hicho kinaendelea kupokea wapiganaji wa demokrasia kutoka pande mbalimbali za nchi wanaovutiwa na dira ya ACT Wazalendo.

“Wapiganaji ambao wamegonga mlango hapa ACT tumekuwa tukiwapokea. Leo ninayo furaha ya kuwaleta mbele yenu wapiganaji wakubwa wawili katika siasa za Tanzania ambao wamepata heshima ya kupokelewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo,” amesema Ado.

Mbali na Ntobi, Ado Shaibu pia alimtambulisha Glory Tausi, ambaye naye ni kada mwandamizi wa CHADEMA aliyeamua kujiunga na ACT Wazalendo.

 Ado amesema wote wameandika barua rasmi za kujiunga na chama hicho, na chama kimewakaribisha kwa mikono miwili.

“Tunao wapiganaji wawili hapa; ndugu yetu Emmanuel Ntobi, mpaka hivi sasa ni kada mwandamizi wa CHADEMA, ameniandikia barua rasmi jana na kusema anayo nia ya kujiunga na ACT Wazalendo. Wa pili ni ndugu Glory Tausi na yeye pia ni kada mwandamizi,” amesema Ado.

Ado Shaibu pia ametoa wito kwa watu wengine wanaotamani kujiunga na ACT Wazalendo kujitokeza, akisema nafasi bado zipo wazi kwa wapigania mabadiliko wenye dhamira ya kweli.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com