Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC SHINYANGA ATOA WITO KWA JAMII KUWALINDA WAZEE


Na WMJJWM- Shinyanga 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ametoa wito kwa jamii hasa Vijana kuwalinda, kuwahudumia na kuwaheshimu wazee katika maeneo yao  badala  ya kuwaachia majukumu ya kulea wajukuu pamoja na kuwafanyia vitendo vya kikatili.

Macha amesema hayo leo Juni 14, 2025 mkoani Shinyanga wakati akifungua Kongamano la Kuelimisha na Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee ikiwa ni sehemu ya  Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha na Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee itakayofanyika Mkoani hapo Juni 15, 2025.

Ameongeza kwamba Serikali inaendelea na jitihada za kuwatunza wazee na kuwaomba wadau na jamii kuendelea kutoa ushirikiano.

"Maadhimisho haya siyo ya Serikali peke yake bali inahitaji ushirikiano wa taasisi na wadau wengine kujitolea kusaidia wazee katika masuala ya matibabu ili waishi maisha yenye staha na utu, wazee msikubali kuachiwa wajukuu na watoto wenu. Kwa sababu ya umri wenu hamuwezi kumudu shughuli ya malezi, nyinyi mliwatunza watoto wenu hakikisheni na watoto wenu wanatunza nyinyi na sio kuwaongezea majukumu ya malezi ya wajukuu" amesema Macha

Akitoa salamu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Naibu Katibu Mkuu  wa Wizara hiyo Felister Mdemu amesema, Wazee ni alama na utambulisho wa Mila na desturi katika Jamii, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anawajibika kuwatunza na kuwahudumia ili vijana wachote busara na hekima zao kwa Ustawi wa Taifa.

"Naomba tuendelee kudumisha heshima kama kipaumbele kwa jamii, kuwajali, kuwahusisha katika shughuli zinazohusu ustawi wa  wazee, kwasababu wazee sio mzigo ni baraka kwa jamii" amesema Mdemu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la  wazee Taifa Mzee Lameck Sendo amesema wazee wanahitaji kulindwa, kuthaminiwa na kutetewa ili waishi kwa furaha na kumalizia maisha yao yaliyobaki hapa duniani.

“Tunahitaji kuwekewa mazingira bora yatakayotufanya tuishi katika utu na usawa kutoka kwenye mamlaka ya Serikali kwani Wazee wanahitaji ulinzi dhidi ya vitendo vya kunyanganywa mali, kuuwawa kikatili na suluhisho ingekua kupatikana kwa sheria moja inayoshughulikia wazee moja kwa moja.” amesisitiza Sendo.

Naye Meneja Miradi kutoka Shirika la Help Age linaloshughulikia Ustawi wa wazee Joseph Mbasa amesema, ni wakati wa kuelimisha jamii hasa vijana kuwatunza Wazee na kupinga ukatili dhidi yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com