
NDOA ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe Brigitte Macron imeendelea kuvuta hisia za watu wengi duniani, huku maswali yakiibuka kuhusu uimara wa uhusiano wao wa muda mrefu unaovuka mipaka ya kawaida ya kijamii.
Hivi karibuni, video iliyosambaa mtandaoni ilimuonyesha Brigitte akimsukuma usoni mumewe Macron wakati walipokuwa wakishuka kutoka kwenye ndege nchini Vietnam. Tukio hilo, lililopewa jina la "Le Slapgate", liliibua gumzo kubwa kuhusu hali ya ndoa yao. Hata hivyo, Rais Macron alilieleza kama utani wa kawaida kati yao, akisisitiza kuwa ni ishara ya ukaribu na si dalili ya mgogoro wa ndoa.
Licha ya matukio kama haya yanayovutia vichwa vya habari, Emmanuel na Brigitte wameendelea kuonekana pamoja kwa ukaribu na mshikamano. Katika mahojiano ya awali, Rais Macron aliwahi kueleza kuwa upendo ni kiini cha maisha yake, na kwamba Brigitte ni sehemu ya mafanikio yake ya kisiasa na binafsi.

Uhusiano wao, ulioanza kwa namna isiyo ya kawaida, umekuwa wa kipekee. Brigitte alikuwa mwalimu wa Macron katika shule ya sekondari, wakati huo Emmanuel akiwa na umri wa miaka 15. Tofauti ya umri kati yao ni miaka 24, jambo ambalo lilikuwa gumu kukubalika kwa jamii na familia zao mwanzoni.
Walifunga ndoa mwaka 2007, baada ya Brigitte kuachana rasmi na mumewe wa kwanza, André-Louis Auzière.
Brigitte, ambaye alizaliwa tarehe 13 Aprili 1953 huko Amiens, Ufaransa, alikuwa ameolewa awali na André-Louis tangu mwaka 1974. Ndoa hiyo ilizaa watoto watatu:Sébastien Auzière (1975), mhandisi wa takwimu,Laurence Auzière-Jourdan (1977), daktari wa moyo na Tiphaine Auzière (1984), wakili
Ingawa Brigitte na Emmanuel hawajazaa watoto wao wenyewe, Rais Macron amekuwa mlezi na baba wa kambo kwa watoto hao, na pia huwathamini wajukuu wao saba kama familia yake binafsi.
Mume wa kwanza wa Brigitte, André-Louis Auzière, alifariki dunia tarehe 24 Desemba 2019 akiwa na umri wa miaka 68. Alijulikana kama mtu wa maisha ya faragha, ambaye hakuwahi kuzungumza hadharani kuhusu uhusiano wa zamani na Brigitte wala maisha ya familia yake.
Kwa sasa, licha ya uangalizi mkali wa umma na vyombo vya habari, Emmanuel na Brigitte Macron wanaendelea kusimama pamoja, wakithibitisha kuwa uhusiano wao ni zaidi ya vichwa vya habari — ni safari ya pamoja iliyojaa majaribu, imani, na upendo wa dhati.

Imeandaliwa na kuhaririwa na Dotto Kwilasa kwa hisani ya mitandao ya kimataifa.
Email_dottokwilasa@gmail.com
Social Plugin