Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKATI BAR INAGEUKA KUWA MTEGO : HADITHI YA WANAUME, POMBE NA MAPENZI YANAYOVUNJA NDOA


Imeandaliwa na Dotto Kwilasa. 

Katika kila kona ya jiji la Dodoma, vipo viti vya plastiki, meza za chuma na chupa zinazo tiririsha jasho la baridi na Mziki unacheza taratibu huku stori za "kijanja" zikipaa hewani,hakuna Shaka ni eneo moja tu linaloitwa Bar.

Lakini nyuma ya ucheshi na furaha ya kwenye bar kuna taswira nyingine mchezo hatari unaohusisha wanaume waliooa na wahudumu wa baa, ambao si tu wanatabasamu kwa huduma, bali pia kwa mkakati wa maisha.

Katika macho ya kawaida, baa ni sehemu ya kupumzika. Lakini jicho langu la tatu linaona mbali zaidi ya chupa na glasi.

Linaona wanaume wanaovaa pete lakini hawavai uaminifu. Linaona wanawake walioajiriwa kuuza bia Bar lakini mwisho wa siku wanajikuta wamebeba huzuni na machozi ya wake wa watu.

Tamaa, Mihangaiko, na Uhalisia wa Maisha ndivyo vinatajwa kuchochea hiyo hali jambo ambalo kwa jicho la tatu ukitazama vizuri linakataa.

Wengi wa wanawake hawa wanavutiwa na hela, hadhi au msaada wa haraka.

Si wote wana nia ovu. Wengine wamekimbia vijijini wakitafuta maisha bora mijini, lakini hatimaye wamejikuta kwenye uwanja wa mapambano ambao silaha ni sura, umbo na busara za kujua “mteja wa kudumu.”

Kwa upande wa wanaume, wengi wao wanaonyesha udhaifu mkubwa wa kisaikolojia na kimaadili. Badala ya kurekebisha matatizo ya ndoa zao, wanakimbilia kwenye baa ambako wanahisi kusikika, kuenziwa, na kupendwa bila masharti ya kuulizwa uko wapi?unafanya nini na mengineyo wakisahau kuwa wengi wanaowapokea huko ni waigizaji wa maisha.

Ni kawaida kumkuta mhudumu wa baa akiwa na mwanaume mmoja jioni ya Jumatano, mwingine Alhamisi na mteja “mkuu” Ijumaa, hili halina ubishi kabisa!

Kila mmoja anaamini ni wa kipekee. Katika ulimwengu wa Bar, kila mwanaume hupewa nafasi ya kuwa shujaa, bila kuulizwa alirudi saa ngapi jana au alipoteza fedha ngapi.

Hili limetengeneza kizazi cha ndoa zinazokufa kimya kimya.

Wake wanapambana kule nyumbani, waume wanapendelewa kule baa. Wengine wanaishia kuhamia kabisa kwa "mrembo wa bar" na kuacha familia zao zikiyumba.

Si kwa sababu wamependa sana, bali wamekimbilia faraja ya muda mfupi isiyohitaji uwajibikaji.

Wanaume wengi waliofungwa kwenye mtego huu ni wale wasiojiamini, waliolemewa na majukumu au wanaotafuta kuhalalisha uzembe wao wa kushindwa kutatua matatizo yao ya kifamilia, wanayakimbia kwa kutumia pombe na wanawake kama bapa la kufunika doa.

Wengine ni walafi wa mapenzi wanaotaka kuheshimiwa nyumbani kama mfalme lakini wanakosa kuwa wafalme wa heshima.

Wanataka kuwa na mke wa ndoa, lakini pia hawakosi “rafiki wa karibu” anayevaa nguo za kubana .

Lakini si kila mhudumu wa baa ni mharibu ndoa. Wapo waliolazimika kubeba maisha mazito kwa vichwa vyao. Wengine ni mama wa watoto wanaotafuta riziki halali,baadhi yao wanateseka kisaikolojia kwa sababu ya mahusiano wanayolazimika kuyakubali ili waendelee na kazi.

Pia wapo wanaume wanaokwenda baa kwa staha kupumzika (hapo ni mmoja Kati ya kumi) kuzungumza na marafiki na kurudi nyumbani bila kuvunja ahadi zao. Lakini wanachohitaji ni kupumzisha akili tu na si mtego wa hisia.

Jicho Langu la tatu Linashauri ndoa nyingi hazifi kwa sababu ya “wanawake wa bar”, bali kwa sababu ya wanaume waliokosa msimamo.

Pia jamii yetu imeshindwa kuwatambua wasichana hawa wa bar kama binadamu wanaohitaji msaada wa kimaendeleo badala yake wameachwa waishi kwa kutumia miili yao kama mtaji.

Ni wakati wa kuhoji si tu tabia za wanaume, bali pia mazingira yanayowafanya wanawake wajione kuwa penzi la mwanaume aliyeoa lina thamani kuliko uhuru wao.

Kikubwa Ndoa zisilindwe kwa maneno matamu, bali kwa uwajibikaji na hofu ya Mungu.

Bar inaweza kuwa sehemu ya furaha, lakini kwa wengi imekuwa kaburi la ndoa. Kwa jicho la tatu, hatuoni tu kinywaji kinachomiminwa tunaona maisha yanavyomiminika taratibu yakitoweka.

Kikubwa wanawake mnaouza Bar jifunzeni kuwa na vya kwenu muepushe maumivu kwa wanawake wenzenu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com