Na Regina Ndumbaro Somanga-Lindi
Katika juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira ya pwani ya Tanzania, Swahili Community Network, kikundi cha wanajamii kinachopatikana Somanga, Wilaya ya Kilwa, kimeonyesha mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa malengo yake ya miaka 2023 hadi 2025.
Kupitia mradi wa NORAD Mangroves unaoratibiwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira WWF Tanzania, kikundi hiki kimefanikiwa kuhamasisha na kuunda vikundi 10 vya mazingira na kupanda mikoko 15,000 kama sehemu ya kulinda mazingira ya baharini.
Swahili Community Network pia imeanzisha vitalu vya mikoko katika kata ya Somanga na Tingi huku wakitoa mafunzo ya kuanzisha vitalu kwa jamii ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi mikoko.
Mafunzo haya pia yamewafikia wakazi wa wilaya ya Mafia na Kilwa, na mpaka sasa miche ya mikoko 30,000 imehifadhiwa.
Kupitia juhudi hizi, jamii imenufaika kwa njia mbalimbali kama vile kuongezeka kwa samaki, kuboreka kwa ardhi na nyasi baharini, hewa safi, pamoja na kupatikana kwa ajira na kipato kwa watu wa kawaida.
Mradi huu haukuzingatia tu mazingira bali pia umejikita katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kutoa elimu ya kilimo cha mwani na ufugaji wa nyuki, pamoja na kuongeza thamani ya mazao hayo kwa kuandaa bidhaa zinazoweza kuuzwa kwa bei nzuri zaidi.
Hili limefungua fursa mpya za kiuchumi kwa wanajamii, hususani wanawake na vijana ambao sasa wanaweza kujitegemea kiuchumi kupitia shughuli hizi.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya, bado kuna changamoto zinazoikumba jamii, ikiwemo elimu duni kuhusu utunzaji wa mazingira hasa kwa kaya zenye kipato cha chini, ukosefu wa rasilimali fedha, na upungufu wa vitendea kazi muhimu kwa uendelezaji wa shughuli hizi.
Swahili Community Network inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kutatua changamoto hizi na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa jamii nzima.

Social Plugin