Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAMCU YAANZA KWA KISHINDO MSIMU WA UFUTA 2025, YAUZA TANI 6,101 MNADA WA KWANZA

ufuta ukiwa ghalani kabla ya mnada kuanza na kutajwa kwa bei rasmi kutoka katika chama kikuu cha Ushirika MAMCU 

Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara 

Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, kinachohudumia wilaya za Mtwara Mjini, Masasi, Nanyumbu na Nanyamba, kimefungua msimu wa mauzo ya zao la ufuta kwa mwaka 2025 kwa mafanikio makubwa. 

Katika mnada wa kwanza uliofanyika wilayani Masasi, MAMCU imewasilisha sokoni jumla ya kilo 6,114,229 za ufuta, sawa na tani 6,101, ambapo bei ya juu ilikuwa Shilingi 2,600 kwa kilo na ya chini ikiwa Shilingi 2,440.

Akizungumza wakati wa mnada huo, Mwenyekiti wa MAMCU, Alhaj Mfaume maarufu kwa jina la Azam Julajula, amesema kuwa mwaka huu chama hicho pia kimefanikiwa kuingiza zao la choroko katika mfumo wa stakabadhi ghalani. 

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, katika mnada wa kwanza, MAMCU imeweza kuuza tani 75 za choroko kwa bei ya Shilingi 1,320 kwa kilo.

Kwa upande wake, Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Mtwara, Ndugu Robert Nsunza, amewataka wakulima kuhakikisha wanazingatia usafi wa ufuta na kuuhifadhi vizuri kabla ya kuupeleka sokoni, ili kuongeza thamani na kuvutia wanunuzi wengi zaidi.

 Amesisitiza kuwa ufuta safi una nafasi kubwa ya kupata bei nzuri katika masoko ya kimataifa.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Rachel Kasanda, amewahimiza wakulima kutumia vyema mapato yatokanayo na mauzo ya ufuta kwa ajili ya kuleta maendeleo katika familia na jamii kwa ujumla. 

Wakulima waliohudhuria mnada huo ameeleza kuridhishwa kwao na mfumo wa uuzaji kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), wakisema kuwa ni mfumo wa haki, uwazi na unaowapa nguvu zaidi wakulima katika kupanga bei ya mazao yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika MAMCU Alhaj Mfaume almaarufu kama azam julajula akiwa katika mnada huo wa ufuta


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com