Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WA MARENDEGO WAOMBA MSAADA KUKAMILISHA NYUMBA YA MGANGA


Baadhi ya Wananchi na Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Somanga Saidi Manjonjo wakikagua nyumba hiyo ambayo bado haijakamilika ujenzi wake
Nyumba iliyojengwa na wananchi wa kijiji cha Marendego iliyopo Kata ya Somanga Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi kwa ajili ya Mganga Mkuu wa Zahanati ya Kijiji hicho
Na Regina Ndumbaro Kilwa-Lindi 

Wananchi wa Kijiji cha Marendego kilichopo Kata ya Somanga, Wilaya ya Kilwa wameiomba serikali ya halmashauri kuwasaidia kukamilisha ujenzi wa nyumba ya mganga katika zahanati yao. 

Wamesema wamejitahidi kwa hali na mali kuhakikisha ujenzi huo unafikia hatua ya umaliziaji, lakini sasa wanahitaji msaada wa serikali ili kukamilisha kazi hiyo muhimu kwa ustawi wa huduma za afya kijijini hapo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Bi Mvita Kilindo amesema juhudi za ujenzi wa nyumba hiyo zimefanikishwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya wananchi na diwani wao. 

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa nyumba hiyo kutamwezesha mganga kuhamia rasmi, jambo litakalorahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa haraka zaidi kwa wakazi wa Marendego.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Somanga, Mheshimiwa Said Manjonjo amewapongeza wananchi wa Marendego kwa moyo wao wa kujitolea na kupenda maendeleo. 

Ameeleza kuwa jamii hiyo imekuwa mfano wa kuigwa kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii. 

Diwani huyo pia ameunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia madirisha na milango ili kusaidia kukamilisha ujenzi wa nyumba ya mganga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com