Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJENZI WA SHULE MPYA YA SEKONDARI MKALI WAWEKA NEEMA KWA WANAFUNZI NA WAZAZI NYASA


Muonekano ya baadhi ya vyumba vya madarasa katika Shule mpya ya Sekondari Mkali kata ya Mkali Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma ambayo imejengwa kwa nguvu za Wananchi kwa kushirikiana na Serikali.
Wanafunzi wa Shule mpya ya Sekondari Mkali kata ya Mkali Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma,wakichukua viti na meza kwa ajili ya kuweka Darasani kabla ya kuanza kwa masomo yao
Baadhi ya Wanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mkali Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma wakiwa Darasani,Serikali kwa kushirikiana na Wazazi imefanikiwa kujenga jumla ya vyumba sita vya madarasa katika shule hiyo ili kuwanusuru wanafunzi wanaotoka kata ya Mkali kutembea zaidi ya kilometa sita kwenda kata ya Liuli na Lundo

Na Regina Ndumbaro Nyasa-Ruvuma 

Wanafunzi wa Shule mpya ya Sekondari Mkali iliyoko katika kata ya Mkali, Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wameanza rasmi masomo yao baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule hiyo. 

Picha mbalimbali zinaonesha wanafunzi wakichukua meza na viti kwa ajili ya kuweka darasani, huku baadhi yao wakiwa tayari darasani wakianza masomo. 

Shule hii mpya imejengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Serikali na hadi sasa ina jumla ya vyumba sita vya madarasa vilivyokamilika kwa lengo la kuwapunguzia wanafunzi wa kata hiyo adha ya kutembea zaidi ya kilomita sita kufuata elimu katika kata za Liuli na Lundo.

Wananchi wa Kijiji cha Mkali wameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo muhimu ambao umeondoa adha ya muda mrefu kwa watoto wao. 

Kwa mujibu wa Isac Mkwera, ujenzi wa shule hiyo ulianza kwa juhudi za wazazi waliochanga Shilingi 3,000 kwa kila kaya ili kufyatua tofali na kununua saruji. 

Serikali ilichangia kwa kutoa bati, rangi, misumari na fedha kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ambapo jumla ya Shilingi milioni 108 zilitumika. 

Kati ya hizo, Sh milioni 50 zilitumika kukamilisha vyumba vinne vya madarasa, Sh milioni 10 kujenga matundu 10 ya vyoo na Sh milioni 48 kwa ujenzi wa vyumba viwili ambavyo vipo hatua ya mwisho kukamilika. 

Mkuu wa shule, Constatino Haule, amesema kazi zilizosalia ni pamoja na uwekaji wa vioo, waya wa mbu, kichomea taka, tenki la maji na chemba.

Wananchi wamesema shule hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya kihalifu, mimba za utotoni na utoro shuleni. 

Eveline Chiwinga ameeleza kuwa awali vijana waliomaliza darasa la saba na kukosa nafasi ya kujiunga na Sekondari walishinda mitaani na kujiingiza kwenye vitendo viovu. 

Kwa upande wake Janeth Mahai, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, ameishukuru Serikali kwa kuleta elimu karibu, akisema kuwa mbali na kupata masomo, wameepuka madhara yaliyokuwa yakitokea njiani ikiwemo kubakwa na kupewa mimba. 

Ameomba Serikali kuongeza vyumba vya madarasa, umeme na miundombinu ya barabara ili kuwezesha mazingira rafiki ya kujifunza, hasa katika masomo ya Sayansi yanayohitaji mafunzo kwa vitendo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com