Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIWANI WA SOMANGA AKABIDHI BATI KWA AJILI YA ZAHANATI YA MARENDEGO


Diwani wa Somanga Mheshimiwa Said Manjonjo akikabidhi bati kwa ajili ya marekebisho ya hitilafu ya kuvuja katika zahanati ya Kijiji cha Marendego kilichopo Kata ya Somanga Wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi
Na Regina Ndumbaro-Kilwa.

Diwani wa Kata ya Somanga, Mheshimiwa Said Manjonjo, amekabidhi bati kwa uongozi wa Kijiji cha Marendego kwa ajili ya ukarabati wa paa la zahanati ya kijiji hicho lililokuwa likivuja. 

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Manjonjo amesema alifahamishwa kuhusu changamoto hiyo na Balozi wa Mtaa Namba 3, nakuchukua hatua ya kufika binafsi kujionea hali halisi kabla ya kuchukua hatua ya kusaidia.

Manjonjo amewahimiza viongozi wa kijiji kuendelea kuwa karibu na wananchi na kufuatilia changamoto zinazojitokeza, ili ziweze kufikishwa kwa viongozi wa juu kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi. 

Amesisitiza kuwa kushughulikia matatizo mapema ni njia bora ya kuboresha huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika maendeleo ya kijiji.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Marendego, Benjamin Mlengela, ametoa shukrani kwa diwani na uongozi wa kijiji kwa kushirikiana kutatua tatizo hilo. 

Ameeleza kuwa mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni zimesababisha paa kuvuja, hali iliyovuruga utoaji wa huduma kwa muda. 

Amesema bati hizo zitarejesha hali ya utulivu na kuwezesha huduma kuendelea kwa ufanisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com