Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAJASIRIAMALI NYASA WAASWA KUTUMIA MIKOPO YA ASILIMIA 10 KUJIKWAMUA NA UMASKINI


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma Khalid Khalif akizungumza na wajasiriamali wadogo kutoka halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma
Baadhi ya Wajasiriamali wadogo kutoka Kata mbalimbali za Wilaya ya Nyasa wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Peres Magiri(hayupo Pichani)wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya vikundi vilivyokidhi vigezo kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Peres Magiri,akizungumza na baadhi ya Wajasiriamali wadogo kutoka kata mbalimbali  Wilayani humo ambao wamekidhi vigezo vya kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya Nyasa,kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Khalif.


Na Regina Ndumbaro Nyasa-Ruvuma 

Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imetenga jumla ya Shilingi 319,831,500 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. 

Katika robo ya pili, Shilingi 189,831,500 zimetolewa kwa vikundi 39 vilivyokidhi vigezo, huku wanawake wakipata Sh.86,800,000, vijana Sh.72,090,000 na watu wenye ulemavu Sh.30,941,000. 

Aidha, katika robo ya tatu, Halmashauri imetangaza kutoa Sh.130,000,000 kwa vikundi vingine 20, huku baadhi ya fedha zikibaki kutokana na waombaji wachache katika kundi la watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa vikundi vilivyopata mikopo hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, amewataka wajasiriamali kuhakikisha wanatumia mikopo hiyo kwa shughuli za kiuchumi na kurejesha kwa wakati ili kuendelea kuwasaidia wengine. 

Amesisitiza kuwa mikopo hiyo ni ya kisheria, ikitokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, na inalenga kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Stella Manyanya, amewapongeza viongozi na watendaji wa Halmashauri kwa kazi nzuri ya kusimamia mapato na kutoa mikopo hiyo. 

Amewataka wananchi kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya matumizi yasiyo ya lazima. 

Mmoja wa wanufaika, Imakulatha Challe kutoka kikundi cha Twaweza, ameishukuru Serikali kwa kuwasaidia kukuza biashara zao kupitia mikopo hiyo isiyo na riba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com