.jpeg)
**
Na Regina Ndumbaro Nyasa-Ruvuma
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Peres Magiri, amewataka Madiwani kushirikiana na Watumishi wa Halmashauri, wakiwemo Watendaji wa Kata na Vijiji, katika kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vile vilivyopo ili kuiwezesha Halmashauri hiyo kujitegemea na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri, Magiri amesema Halmashauri yenye vyanzo vingi vya mapato itakuwa na uwezo wa kukusanya fedha nyingi ambazo zitatumika kuboresha huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha, Magiri amewasisitiza Madiwani kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato unaenda sambamba na nidhamu ya matumizi ya fedha.
Amewataka wasimamie matumizi ya mapato yanayokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa kupitia kamati zao, Madiwani wanapaswa kufuatilia na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao kwa lengo la kujiridhisha na thamani ya fedha inayotolewa na Serikali.
Pia amewataka watumishi wapya kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, na kuepuka tabia zinazoweza kuzua migogoro na kuchochea chuki kati ya Serikali na wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Khalid Khalif, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri hiyo imepangiwa kukusanya Shilingi bilioni 2.4, ikiwa ni ongezeko la asilimia 66 kutoka mwaka uliopita.
Hadi kufikia tarehe 30 Machi 2025, Halmashauri ilikuwa imekusanya Shilingi bilioni 1.8 sawa na asilimia 78.36, na kufikia Aprili 28, ilikuwa imekusanya zaidi ya asilimia 82 ya mapato ya ndani yaliyopangwa.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri hiyo imepangiwa kukusanya Shilingi bilioni 3.2, sawa na ongezeko la asilimia 35.
Mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuwekeza katika uchimbaji wa makaa ya mawe, kununua leseni 20 za uchimbaji na kutenga Shilingi milioni 20 kwa ajili ya biashara ya makaa hayo.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Stella Manyanya, amepongeza ushirikiano baina ya watumishi wa Halmashauri katika kipindi cha miaka mitano (2020–2025), hali iliyosaidia kuvuka malengo ya ukusanyaji mapato ya ndani na kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Zefania Manyeshi, ameipongeza Halmashauri kwa kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Stewart Nombo, amewataka Madiwani kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ili Serikali ieleweke vyema kwa wananchi.
Social Plugin