Na Hamida Kamchalla, TANGA.
MAKAMU Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Taifa Isihaka Mchinita amesema upinzani kususia uchaguzi ni kutoa nafasi kwa chama tawala Ccm kuendelea kuongoza jinsi wanavyotaka wao badala yake ni kupambana kwa kukupigania haki ya Watanzania ili kupata viongozi halali.
Mchinita ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumzia na watia nia wa nafasi mbalimbali za uongozi jijini Tanga na kusema ACT hawajasusia uchaguzi.
"Ushahidi wa kihistoria unaonesha kuwa pale kila pale tunapoamua kutoshiriki, utawala wa mabavu ulitumia mazingira hayo bora kwao, kuboresha ukandamizaji na kuweka mazingira ya kuendelea kuwadhulumu watu kwenye nchi, kwasababu hakuna anayekabiliana nao,
"Hivyo Halmashauri kuu ACT ikaamua kwamba tutashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 huku tukiendeleza mapambano ya kudai heshima na thamani ya kura ambayo ilipotea, na tukikubali kupoteza heshima yetu ni kukubali kuwa watumwa kwenye Taifa letu", amesema.
Aidha amesema, Taifa linahitaji kuwa na viongozi wenye weledi lakini pia hofu ya Mungu ili waweze kuwatumikia na kuwajali wananchi wake jambo ambalo litaiweka nchi huru pasi na migongano ndani ya siasa.
"Inafikia mahali viongozi hawahitahi hata kupigiwa kura na wananchi wake, ni kwamba hawana hisia za kupigania haki na ustawi wa wananchi hao, na ndiyo hali iliyopo, lakini hali hiyo haiwezi kuondoka kwa sisi kukaa pembeni,
"Chama chetu kimeona kuwa namna pekee ya kutoka hapa ni lazima tukapiganie na kufanya operesheni hii ya demokrasia kuwa ndio muelekeo wa chama chetu na tuwaeleze wananchi kuwa kupigania heshima na haki zao ni wajibu wao", amesisitiza.
Naye John Mbogo, mtia nia kuwania kiti cha Ubunge Tanga mjini amesema wamefarikika sana kwa ujio wa kiongozi wao Kitaifa kwani imewaamshia ari ya wananchi waliokata tamaa kwa chama chao katika kupaza sauti zao.
"Tumepita katika kata 17 kati ya 27 za Jimbo hili na ari ya wananchi katika kushiriki zoezi zima la kupiga kura imeshuka kwa zaidi ya asilimia 50, kwahiyo ni wachache sana ambao wana kiu ya kujihusisha katika zoezi hili,
"Sasa ziara hii ya Makamu Mwenyekiti wetu inatupa amsho, lakini pia kuna maneno ambayo tumekuwa tunatembea nayo kwamba 'uhondo wa nhoma uingie ucheze' na sisi siyo watu wa kususa, hasa watu wa Tanga hatuna desturi hiyo", amesema Mbogo.
Kwa upande wake mtia nia wa kiti cha udiwani kata ya Central Zainab Mahanyu ameeleza kuwa yapo mambo kadhaa yaliyomsukuma kuwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha ACT ambayo yanechangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma kimaendeleo Mkoa wa Tanga.
Amesema Mkoa huo ulikuwa ni lango la biashara pamoja na wafanyakazi kwamaana ya viwanda ambayo kwasasa vingi vimekufa huku vingine vikiuzwa kwa wawekezaji ambao mbali ya hivyo havijaendelezwa na kuacha magofu
Social Plugin