Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SOSTHENES KATWALE APEWA BARAKA ZA CCM KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA SOLWA

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha Mtaalamu wa Mipango na Usimamizi wa Maendeleo, Sosthenes Julius Katwale, kuwa mgombea wake wa Ubunge kwa Jimbo la Solwa mkoani Shinyanga katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Katwale alianza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Kashishi, iliyoko Solwa, kabla ya kujiunga na Sengerema Seminary na baadaye Makoko Seminary kwa masomo ya sekondari, akitokea Parokia ya Salawe.

 Anaingia kwenye kinyang’anyiro hiki akiwa na uzoefu mkubwa wa kitaaluma na kikazi katika sekta za mipango, usimamizi wa ardhi, sera, na maendeleo ya jamii.

Amebobea kitaaluma akiwa na Shahada ya Kwanza ya Mipango na Usimamizi wa Mazingira kutoka Chuo cha Mipango Dodoma, Shahada ya Uzamili ya Mipango na Usimamizi wa Miji kutoka Chuo Kikuu Ardhi, na kwa sasa yupo katika hatua za mwisho za Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Usimamizi wa Sera na Mipango kutoka SUA.

Mbali na elimu, Katwale amepitia mafunzo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ikiwemo China, Ujerumani, Uholanzi, Namibia, Rwanda na Ethiopia. Mafunzo haya yamejikita kwenye maeneo ya matumizi bora ya ardhi, usimamizi wa miradi, tafiti zenye tija, na matumizi ya mifumo ya kisasa ya upangaji na ufuatiliaji wa bajeti za serikali.

Kitaaluma, Katwale ni Mhadhiri wa Chuo cha Mipango, Mwanza tangu mwaka 2017 hadi sasa, na awali alihudumu kama Mhadhiri katika Chuo cha Mipango Dodoma (2011-2017).

Vilevile amewahi kuwa mshauri wa vyuo vikuu barani Afrika na mshiriki katika mijadala ya kimataifa kuhusu utawala wa ardhi kupitia wizara ya ardhi na taasisi za kifedha za kimataifa kati ya mwaka 2017 hadi 2021.

Kwa msingi wa uzoefu wake wa kitaalamu na ukaribu wake na wananchi wa Solwa, Katwale ameahidi kuwa sauti ya wanyonge bungeni na kushirikiana na serikali katika kusukuma mbele maendeleo endelevu ya Jimbo hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com