MNEC Joseph Peneza akiwa katika mkutano Wilayani Nanyumbu Mkoani Mtwara
Na Regina Ndumbaro - Mtwara.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka Mkoa wa Mtwara, ndugu Joseph Peneza, amechangia shilingi milioni 2.5 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wilayani Nanyumbu.
Mchango huo umetolewa aliposhiriki Baraza la Jumuiya ya Wazazi CCM wilayani humo, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Akiwa katika ziara hiyo, ndugu Peneza amekagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba hiyo na kushiriki moja kwa moja katika ujenzi wa msingi wa nyumba hiyo.
Mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo, ndugu Peneza ameonesha kuguswa na juhudi zinazofanywa na jumuiya hiyo na kuahidi mchango huo mkubwa ili kuona mradi huo unakamilika kwa wakati.
Ameeleza kuwa kama kiongozi wa kitaifa, ni wajibu wake kusaidia juhudi za maendeleo katika ngazi ya chini kwa lengo la kuimarisha ustawi wa jumuiya na chama kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, ndugu Peneza amechangia viti 50 kwa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Nanyumbu kwa lengo la kuwawezesha kuongeza kipato chao kupitia shughuli za mikutano na kumbi za matumizi mbalimbali.
Amesema kuwa michango hiyo ni sehemu ya mwitikio wake wa kusaidia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ndani ya jumuiya, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika hotuba yake la Baraza hilo, ndugu Peneza amewataka wanajumuiya na wananchi kwa ujumla kuendelea kuiunga mkono serikali ya CCM kwa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo.
Pia amewahimiza kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Nanyumbu, ndugu Alphonce Luoga, amemshukuru ndugu Peneza kwa kukubali mwaliko wa kushiriki baraza hilo na kwa msaada alioutoa.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Bi Mary John Mchopa, amemuahidi MNEC Peneza kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa na kuyafanyia kazi kwa maslahi ya jumuiya na maendeleo ya chama kwa ujumla.
Muonekano ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara
Social Plugin