Picha : RC MACHA AONGOZA MBIO ZA SHYCOM ALUMNI MARATHON 2024...APONGEZA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI



Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MBIO za Shycom Alumni Marathon 2024, ambazo zimeandaliwa na wanafunzi waliowahi kusoma chuo cha ualimu Shinyanga (SHYCOM), ambacho zamani kilikuwa chuo cha biashara zimetamatika, huku Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akipongeza mbio hizo.

Mbio hizo zimefanyika leo Septemba 21,2024 katika viwanja vya michezo CCM Kambarage Manispaa ya Shinyanga, ambapo washiriki wamekimbia mbio za kilomita 5,10 na 21, pamoja na kufanyika mashindano ya mbio za baiskeli.


Macha akizungumza kwenye mbio hizo, amesema tukio hilo ni la kihistoria ambapo wanafunzi waliowahi kusoma katika chuo hicho wameonyesha uzalendo mkubwa, kwa kuungana kwa pamoja na kuanzisha Marathon hiyo, ili kupata fedha za kuboresha miundombinu ya chuo na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya elimu na kuimarisha afya kupitia michezo.

“Tukio hili la Shycom Alumni Marathon ni la kihistoria hapa Shinyanga, nawapongeza sana wanafunzi ambao mliwahidi kusoma katika chuo hiki kwa uzalendo wenu wa kukusanyika na kufanya tukio hili, ili kupata pesa za kuboresha mazingira ya chuo ambacho mlisoma na kupata elimu,”amesema Macha.

“Chuo hiki mmetoa hazina kubwa ya wasomi hapa nchini wakiwamo Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG), Profesa Charles Kichere na aliyestaafu Prof Mussa Assad na leo mpo hapa nawapongeza sana kwa uzalendo wenu na tukio kama hili, naomba liwe mfano wa kuigwa kwa watu wengine kukumbuka fadhila kwa shule na vyuo walivyosoma ikiwamo na shule ya sekondari Shinyanga (SHYBUSH) watafutane na kufanya kitu,”ameongeza.

Amesema mbio hizo pia zimesaidia kukuza uchumi wa mkoa wa Shinyanga, sababu wageni kutoka maeneo mbalimbali waliwasili mkoani humo na kupata huduma mbalimbali zikiwamo za maradhi.

Jesca Domick akisoma risala kwa niaba ya wana umoja wa Shycom, amesema walikutana na kuamua kuanzisha mbio hizo za hisani Shycom Alumni Marathon, kwa lengo la kupata fedha ili kuboresha miundombinu ya chuo hicho kama kurudisha fadhila, na kwamba kila mwaka kutakuwapo na mbio hizo ikiwa na lengo pia la kuibua vipaji vya wakimbia riadha.

Mkuu wa Chuo cha Ualimu SHYCOM John Nandi, amepongeza mbio hizo, kwamba fedha ambazo zimepatikana zitakwenda kuboresha miundombinu ya chuo hicho, hali ambayo itasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa mafunzo.

Mmoja wa washiriki wa mbio hizo Joseph Panga, ambaye ameshinda mbio za kilomita 21,amesema mashidano hayo ni muhimu kwa sababu yanakuza vipaji vya watu wengi pamoja na kupata ajira.



































































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post