MBUNGE RWEIKIZA AJIVUNIA UTEKELEZAJI WA MIRADI MINGI NA MIKUBWA JIMBO LA BUKOBA VIJIJINI

 
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza akielezea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi wakati wa kikao cha halmashauri kuu

Na Mariam Kagenda _Kagera 

Mbunge  wa Jimbo la Bukoba Vijijini mkoani Kagera  Dkt Jasson  Samson Rweikiza amesema kwa kipindi cha miaka 3 (2021_2023) miradi mingi ya Maendeleo imetekelezwa hasa kwenye sekta za Miundombinu ikiwemo  Barabara, Elimu na  Afya kwa kata zote za Jimbo hilo.

Dkt Rweikiza amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka 3 wakati wa kikao cha kawaida cha Halmashauri kuu ya Chama hicho wilaya ya Bukoba Vijijini ambacho kimefanyika April 20 katika Jimbo hilo.

Ametaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa katika jimbo hilo kwa kipindi hicho  kuwa ni pamoja na miradi ya Barabara ambapo kwa mwaka wa Fedha 2020/2021 miradi 52 ya Barabara katika kata 29 zilifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara , utengenezaji maeneo korofi pamoja na matengenezo ya madaraja madogo ikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1, na kwamba Mwaka 2021/2022 Miradi 50 ya Barabara yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2 ilitekelezwa katika kata 29.

Ameongeza kuwa kwa mwaka wa Fedha  2022/2023 miradi ya Barabara 48 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1 katika kata 29 imetekeleza na kwa mwaka wa fedha 2023/2024 mpaka taarifa hiyo inaandaliwa miradi 4 kati ya 52 ya barabara ambayo inatekelezwa ilikuwa imekamilika ambapo miradi 48 inaendelea na ukarabati na mingine iko katika hatua za manunuzi na fedha zote zinatoka katika mfuko wa barabara , Fedha za Jimbo na tozo za mafuta ili kukamilisha kazi.

Dkt. Rweikiza amebainisha kuwa miradi mingine iliyotekelezwa katika Jimbo hilo ni miradi ya afya na Elimu ambapo zimejengwa Zahanati na kuboresha huduma za afya na wanaendelea na ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Rukoma  sambamba na ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari.

Amesema kuwa katika kipindi hicho pia miradi ya maji imetekelezwa katika kata ya Kagya, Katoma, Karabagaine , Kemondo, Katerero na Bujugo akieleza kuwa mafanikio hayo ni kutokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi, Serikali pamoja na Mbunge huku akimshukuru Mh Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi ya utekelezaji wa miradi mikubwa katika Jimbo hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Kagera Nazir Karamagi aliyekuwa  mgeni Rasmi katika kikao hicho amewataka wanachama wa chama hicho kuwapa ushirikiano viongozi walioko madarakani na kutowasumbua kwani kipindi cha uchaguzi bado isipokuwa wawape ushirikiano ili waweze kutekeleza ilani ya chama hicho kama walivyowaaidi wananchi .

Naye mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi  Taifa  (MNEC)  Bwana Kharim Hamri amewataka wanachama wa chama hicho kuwapuuza watu wanaotafuta madaraka kwa mafarakano au misingi ya udini na ukabila kwani hatowafaa kuwa kiongozi wao na kuongeza kuwa chama hicho kiko imara na viongozi wake wanaendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa ili kuwaletea wananchi maendeleo.   
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza akisoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi wakati wa kikao cha halmashauri kuu
MNEC Karim Hamri akizungumza na wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Bukoba Vijijini wakati wa kikao cha halmashauri kuu
Wajumbe wa halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi wilaya ya Bukoba Vijijini

Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza akisalimiana na  Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Kagera Nazir Karamagi





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post