Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAHAFALI YA TANO LITTLE TREASURES SECONDARY YANG’ARA, WAZAZI WAHIMIZWA KUWEKEZA KWENYE ELIMU

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mahafali ya Tano ya Shule ya Sekondari Little Treasures iliyopo Mjini Shinyanga yamefanyika kwa uzito mkubwa na hamasa ya kipekee, yakikutanisha wazazi, walimu, viongozi na wadau mbalimbali wa elimu katika Mkoa wa Shinyanga.

Hafla hiyo iliyofanyika Desemba 5,2025 imeonesha ukubwa wa uwekezaji wa shule hiyo katika kuinua kiwango cha elimu na kujenga kizazi chenye maadili, maarifa na uwezo wa kutimiza ndoto zao.

Akiwasilisha risala ya mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Little Treasures, Alfred Mathias, alisema jumla ya wanafunzi 61 wamehitimu masomo yao, wakiwemo wavulana 36 na wasichana 25, huku akisisitiza kuwa shule hiyo itaendelea kujenga misingi imara ya nidhamu na ufaulu.

Mkurugenzi wa Shule za Msingi na Sekondari Little Treasures, Lucy Mwita, alisema wamejidhatiti kuendelea kuwa hazina ya watoto na daraja la mafanikio kwa kuwajengea uwezo, maadili na uelewa mpana wa masomo yao.
Aliwataka wazazi kuendelea kuiamini na kuiunga mkono shule kwa kupeleka watoto wao ili waendelee kupata elimu bora.

Kwa upande wake, Meneja wa shule hiyo, Wilfred Mwita, alisema Little Treasures itaendelea kujituma kwa bidii kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa kwa weledi na kuandaliwa kufikia malengo yao ya kitaaluma na maisha, huku akiomba mashirikiano zaidi kutoka kwa wazazi.

Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bakari Ally, aliwataka wazazi kubadili mtindo wa maisha na kuacha kuendekeza starehe zinazopoteza fedha, badala yake wawekeze kwenye elimu ya watoto wao.
Bakari alisema wazazi wengi wamekuwa wakitumia fedha nyingi kwenye sherehe za ubatizo hadi shilingi milioni 3 au sherehe za siku ya kuzaliwa kwa zaidi ya laki 8, lakini wanapofika Januari wakitakiwa kulipia ada za watoto wao, huanza kuomba muda na kusisitiza kuwa hawana fedha.

“Wazazi wekeni vipaumbele vyenu kwenye mambo muhimu na kuacha kupoteza pesa hovyo. Sasa hivi ni mwezi Desemba lakini mtu anafanya sherehe ya ubatizo shilingi milioni 3, au sherehe ya kuzaliwa shilingi laki 8. Ikifika Januari unadaiwa ada unasema huna hela, hivi unadhani walimu watakuelewa kweli?” alisema.
Alisisitiza kuwa elimu ni uwekezaji na wazazi hawapaswi kuchelewesha ada za watoto wao.

“Maji ukiyavulia nguo lazima uyaoge, lipeni ada kwa wakati. Ukweli mchungu, lakini wazazi badilini mtindo wa maisha ,kusomesha mtoto ni kufanya uwekezaji,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Bakari aliitaka Shule ya Sekondari Little Treasures kuanzisha Club ya Sheria, ambayo itakuwa ikipokea wataalamu wa sheria kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwa ajili ya kutoa elimu ya sheria shuleni hapo na kuwajengea wanafunzi uelewa mpana wa masuala ya kisheria.

Aliwataka wahitimu kuendelea kudumisha nidhamu, kuwa mabalozi wazuri wa shule hiyo na kuitangaza vyema popote watakapokwenda.
Sehemu ya wahitumu wakicheza muziki

Mtendaji wa Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Bakari Ally akizungumza.
Mkurugenzi wa Shule za Msingi na Sekondari Little Treasures Lucy akizungumza.
Meneja wa shule za Little Treasures Wilfred Mwita.
Mkuu wa shule ya Sekondari Little Treasures Alfred Mathias akisoma Risala ya shule.
Mwakilishi wa wazazi aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza.

Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akimpongeza mtoto wake Cedric kwa kuhitimu kidato cha Nne shule ya Sekondari Little Treasures.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com