MAVUNDE AWAKOSHA MAMA, BABA LISHE DODOMA, AWAPA MAJIKO YA GESI 500

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde akiwa amekumbatiwa na mmoja wa mama lishe waliobahatika kupata fursa ya jiko la gesi kama ishara ya kushukuru. 

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog, Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini Anthony Mavunde amegawa majiko ya  gesi 500 kwa Mama Lishe na Baba Lishe wa Jijini Dodoma ikiwa ni hatua yake ya kuchochea uchumi kwa Wajasiriamali ili kuboresha shughuli zao na kuinua kipato chao. 

Akizungumza kwenye zoezi hilo jijini hapa amesema anaamini majiko hayo yatachochea zaidi shughuli za kiuchumi kwa Wajasiriamali hao na hivyo kuboresha shughuli zao za kipato cha kila siku.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa juhudi zake hazitaishia hapo na badala yake yeye kwa kushirikiana na wadau mbalimbali  ataandaa utaratibu wa upatikanaji wa mitambo ya kutengeneza mkaa mbadala(briquette) na kugawa kwa vikundi vya wakina Mama na vijana. 

"Naamini hatua hii itasaidia kuboresha maisha ya watanzania wa kipato cha chini ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira yetu ambayo yapo hatarini kutokana na uharibifu wa ukataji miti hovyo kwa ajili ya mkaa, " Amesema
Mavunde pia ametumia nafasi hiyo kuwataka wajasiriamali wa Jiji la Dodoma kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo Dodoma na hasa kuzingatia ukuaji wa kasi wa Jiji baada ya maamuzi ya Serikali kuhamishia shughuli zake zote Dodoma.

Mbunge huyo amesema nafasi hiyo ni yakipekee ambayo wanadodoma wanapaswa kuichangamkia badala ya kuwa watazamaji wa fursa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amepongeza zoezi la ugawaji majiko hayo kwa wajasiriamali huku akitoa elimu ya matumizi ya majiko hayo ili yasilete athari baadaye.

"Kuna watu hawataki kutumia majiko ya gesi kwa kudhani kuwa yana madhara,inatakiwa kuwa waangalifu wakati wa matumizi yake, ukisikia harufu kama ya yai viza hakikisha unafungua madirisha yote ya nyumba na kufunga vizuri jiko lako kabla ya kuliwasha, " Amesema

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ORYX Benoit Araman amesema Kampuni yake inaunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu  Hassan za matumizi ya nishati safi kwa wananchi ili kuokoa mazingira. 

 "Tunatambua umuhimu wa kutunza mazingira hivyo tutaendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kutimiza lengo la 80% ya matumizi ya nishati safi kwa wananchi ifikapo mwaka 2032," Amesisitiza Mkurugenzi huyo . 
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post