MADINI KUWEKA MIKAKATI SHIRIKISHI UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI





# Kushirikiana na Makampuni bingwa ya Ushauri nchini kuitangaza sekta ya madini

# Wizara ya Madini kufungua Dawati maalum la Uwekezaji TIC

*Kufungua kiwanda cha uchenjuaji kitakacho hudumia  Ukanda wa Sub Sahara Afrika

Wizara ya Madini imepanga kuweka mikakati shirikishi  ya uwekezaji katika Sekta ya madini itakayowavutia na kuwanufaisha wachimbaji wadogo,wa kati na wakubwa.

Hayo yamebainishwa Novemba 21, 2023  na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali wakati akizungumza na uongozi wa kampuni ya BHP na Lifezone katika mkutano wa biashara  baina ya Tanzania na Uingereza unaoendelea jijini London.

Sambamba na hapo, amesema wizara ya madini itaandaa mpango wa mafunzo maalum yaani _Apprenticeship Program_ katika maeneo kazi kwa maafisa ili kuongeza ujuzi na maarifa kwenye mnyororo mzima wa uwekezaji ndani na nje ya nchi.

Mahimbali ameongeza kuwa , wizara ya madini kwa kushirikiana na kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) itafungua Dawati maalum la  uwekezaji kwa ajili ya kuratibu shuguli za  uwekezaji ndani ya sekta ya madini.

Akielezea kuhusu ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji madini mkakati, Mahimbali ameeleza  kuwa Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya _BHP Group Limited_ na _Lifezone Metals_ kupitia kampuni tanzu ya Tembo Nickeli imepanga kujenga kiwanda kikubwa nchini Tanzania cha uchenjuaji madini mkakati yatakayochimbwa katika nchi zilizo Ukanda wa Sub Sahara Afrika.

Akiwa ameambatana na wataalam kutoka wizara ya madini, Mahimbali amesema kuwa Wizara ya Madini imeridhishwa na mwamko ulioneshwa na wawekezaji wa nchini Uingereza na kuahidi kutoa kushirikiana mzuri  kwa faida ya nchi zetu.

Akizungumzia maendeleo na ukuaji wa sekta ya madini nchini , Mahimbali amebainisha kuwa kwa mwaka 2022 Sekta ya Madini imekuwa kwa asilimia 10.9 na imechangia asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa na kuingiza asilimia 56 ya fedha zote za kigeni nchini.

Aidha, akielezea kuhusu mafanikio ya ziara hiyo, Mahimbali amesema kuwa timu ya wataalam imejifunza mambo mbalimbali ya kibiashara ikiwemo  umuhimu wa wachimbaji madini kuwa na taarifa nzuri za biashara zinazoweza kushawishi uwekezaji , kuongeza uratibu wa takwimu za kitaifa zinazohusu sekta ya madini na  kuwajengea ujuzi na maarifa  maafisa ili waweze kuhudumia wawekezaji kwa kiwango kinachotarajiwa kimataifa.

Vilevile, Mahimbali amewashukuru watanzania wanaoishi nchini Uingereza (Diaspora) kwa ushirikiano wao waliouonesha katika kufanikisha ziara hii na kuaahidi kuwa wizara itateua Afisa Dawati Maalum la Madini ambaye atakuwa ndani ya Kituo cha Uwekezaji kwajili ya kushughulikia uwekezaji sekta ya madini.

VISION 2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post