WAZIRI MAVUNDE AIBUKIA KWENYE SOKO LA DHAHABU KAHAMA USIKU UTOROSHAJI MADINI, AFUNGA LESENI ZA KAMPUNI YA NADOYO
Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog Kahama.

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde (MB), amezifungia leseni zote za Kampuni ya Nadoyo Mineral Trading Company kujihusisha na biashara ya madini nchini,  kufuatia kukamatwa kwa mmoja wa pande zinazohusika na kampuni hiyo, zikijaribu kutorosha Dhahabu yenye uzito wa kilo 4.3, zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 562,288,207 katika mkoa wa kimadini Kahama.

Waziri Mavunde amefanya maamuzi hayo jana Oktoba 11, 2023 majira ya usiku, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika soko la madini Kahama, baada ya kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, aliyekamatwa juzi Oktoba 10 kati ya saa 1 hadi saa 4 usiku katika eneo la Niteshi mjini Kahama.

“Kufuatia tukio hili, ninamwagiza katibu mtendaji wa tume ya madini, kusimamisha mara moja leseni zote za mfanyabiashara huyu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa, na hii iwe fundisho kwa wafanyabiashara wengine wenye nia ovu ya kuhujumu uchumi wa nchi yetu” ,alisema Mavunde

“Kuanzia sasa hivi, mtu au Kampuni au kikundi chochote kitakachobainika kutaka kutorosha madini adhabu ya kwanza ni kufungiwa leseni nchi nzima, hawezi mtu kuhujumu Kahama halafu akaendelea na biashara hiyo hiyo sehemu nyingine, haiwezekani, lazima tutakufungia na mahakama ikikukuta na hatia, nakushauri tafuta biashara nyingine ya kufanya maana huku hapatakufaa kabisa na hatua zitachukuliwa bila kujali wadhfa wa mtu” Alisisitiza 

Sambamba na hilo, Mhe. Mavunde alitoa wito kwa wafanyabiashara wa madini nchini kupitia wafanyabiashara wa Kahama, kuwa wazalendo kwa kufuata taratibu zilizopo na kulipa tozo, ada na kodi mbalimbali ili kuiwezesha Serikali kupata mapato na kuendelea kuimarisha huduma kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara, umeme, afya na elimu.

Kupitia mkutano huo na waandishi wa habari, uliohudhuriwa pia na baadhi ya wafanyabishara wa madini-Kahama, waziri Mh Mavunde aliwasihi vijana kuchangamkia fursa ya madini, kwani wizara hiyo tayari imefanya mazungumzo na umoja wa mabenki nchini, ili kuhakikisha sekta hiyo inakopesheka na kwamba milango ipo wazi ili vijana waweze kuongeza mitaji na wafanye kazi zao vizuri.

“Wizara yangu pamoja na umoja wa mabenki nchini, tumejifungia ndani siku nzima, nikitaka kujua kwanini sekta hii huwa haikopeshwi, lakini niwahakikishie kwamba sasa mtakopesheka, muongeze mitaji yenu, na mfanye kazi zenu vizuri zaidi” ,alisema Mavunde


Pia, Mheshimiwa Mavunde alionesha utayari wa kutenga siku na kukaa pamoja na wafanyabiashara wa madini ili kwa pamoja wamweleze hasa ni nini wanadhani inaweza kuwa ni changamoto kubwa inayopelekea baadhi yao kufikia hatua ya kujihusisha na vitendo vya utoroshaji madini, hatua ambayo anaamini itasaidia Serikali kuchukua njia sahihi kushughulikia suala hilo.

Vilevile, Mheshimiwa Mavunde alieleza bayana kuwa pamoja na hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watoroshaji wa madini, pia madini yote yatakayokamatwa yatahifadhiwa na Serikali na kupelekwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kusubiri hatma ya Mahakama.

Awali, akieleza taarifa ya masoko ya dhahabu, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Madini Kahama, Bw. Jeremiah Hango alibainisha kuwa takribani kilo 562.3 za dhahabu, zenye thamani ya shilingi bilioni 74.8 ziliuzwa katika masoko na vituo vya madini kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01 Julai, 2023 hadi 10 Oktoba, 2023.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mheshimiwa Mboni Mhita alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, na kuahidi kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha vitendo vyote vya utoroshaji wa madini vinakomeshwa.

Endapo kama madini hayo yangefanikiwa kutoroshwa, serikali ingepoteza kodi ya takriban milioni 50, ambapo ndani yake kuna mrabaha, Ada ya ukaguzi, Ushuru wa huduma na kodi ya mapato TRA.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post