TSB YAWAFUNDA WAWATA KUHUSU KILIMO, FURSA NA MASOKO YA MKONGE

 
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), imetoa elimu ya kilimo cha zao la Mkonge, masoko na fursa zitokanazo na zao hilo kwa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), katika Semina ya kuhitimisha kongamano la Wawata Kanda ya Mashariki jijini Tanga.

Akizungumza kwenye semina hiyo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Zao la Mkonge na Masoko wa TSB, Olivo Mtung’e, amesema Bodi hiyo ambayo pia ni mdhamini wa kongamano hilo, imeona ni vema kuwashirikisha wanawake Wakatoliki kwenye katika suala zima la kuinua kipato chao na kujiimarisha kwenye familia kwa sababu wao ndiyo wasimamizi wa familia.

“Kama tunavyofahamu zao la Mkonge ni zao ambalo linavumilia sana ukame hasa ukizingatia sasa hivi tunapambana na hili tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa Kanisa Katoliki wao walishaanza tangu mwaka 2015 kuzungumzia jambo hili ambapo Papa Francis alitoa waraka unaozunguzmia namna ya kukabiliana na changamoto hii ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Kwa leo tumezungumza mambo machache tu kwamba miaka mitatu iliyopita tumekuwa na shida ya mvua na mazao mengi ambayo yanategemea sana mvua yalikuwa ya shida hata bei za vyakula zilipanda. Kwa hiyo Wawata wao tumewashauri kwenye mashamba yao ya kawaida wapande kama uzio baadaye watavuna na kupata pesa za kulisha familia zao. Lakini wanaweza kupanda katika mazao yao wakapanda kama uzio au mpaka lakini yakawa chanzo cha pesa ambacho kinaweza kusaidia familia,” amesema.

Mtung’e amesema lengo la kuwakaribisha Wawata kwenye kilimo kwa maana hiyo ya faida hizo zilizotajwa kwamba unaweza ukawa ni uzio au mpaka, lakini pia Mkonge wenyewe unarutubisha ardhi ambapo Wachina wameanza kulima milimani kwa ajili ya kukabiliana mabadiliko ya tabia nchi kwamba yenyewe inahifadhi mazingira lakini zao la Mkonge lenyewe halina msimu.

Kutokana na hali hiyo, amesema pia wanaweza wakaingia katika hatua ya pili ya ujasiriamali tunafahamu wanawake sasa hivi  wana vitu vingi vikiwamo vikundi vya ujasiriamali ambapo wanaweza wakafuma mazuria, vitambaa vya mezani (table mats) kwa ajili ya kuuza.

“Rais wetu Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan amefungua nchi yeye amefungua nchi kwa mataifa mbalimbali kupitia filamu yake ya Royal Tour sasa watalii wanakuja. Ukiangalia Mkonge na bidhaa zake ni za asili kwa hiyo wenzetu wanaokuja kutoka mataifa mbalimbali wanategemea waje Afrika ambako watapata vitu vya asili.

“Kwa hiyo mwanamke anao uwezo wa kuzipata hizo bidhaa akazitengeneza akapata pesa hata za kigeni kupitia hao watalii watakaokuja nchini. Lakini pia wale wanaoweza kuingia moja kwa moja kwenye biashara kwa maana tuna wakulima wengi ambao wameingia kwenye kilimo hilki ambapo wanazalisha, wanasindika sasa na wenyewe wanaweza kuingia kwenye ule mnyororo wa thamani kwa maana ya kununua na kuuza na wakawa wanendelea kuimarisha familia zao,” amesema.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Wawata Kanda ya Mashariki, Theodora Mtegeta amesema Bodi ya Mkonge Tanzania ni mkombozi wa mwanamke ikiwa kama kikundi au mmoja mmoja na kuongeza kuwa hata yeye ni shahidi ambapo ana shamba amelima Mkonge hivyo anajua hela ya Mkonge ilivyo tamu.

“Kwa hiyo kinamama wengine wamehamasishwa leo tunamshukuru Mkurugenzo Olivo kwa kutupitisha kwenye kilimo, akatupitisha kwenye masoko, fursa zilizopo kwenye Mkonge, mashamba yapo na hata kama una shamba lako au la familia unaweza kulima mkonge. Kwa hiyo tumepata somo zuri sana kinamama,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post