WANANCHI WAFUNGA OFISI YA KIJIJI

 

Wananchi wa kijiji cha Ngelenge kilichopo katika kata  ya Ruhuhu wilayani Ludewa mkoani Njombe, wameifunga ofisi ya mwenyekiti wa kijiji hichoThomas Mkinga wakidai kuwa anahujumu uchumi wa kijiji na kumtaka ajiuzulu.


Wakizungumza wananchi wa eneo hilo akiwemo Frolence Haule amesema kuwa mwenyekiti huyo amekuwa akikusanya pesa za ushuru na kufanyia matumizi yake binafsi na wanapohitaji mikutano ya taarifa ya mapato na matumizi hataki kuitisha huku Avelina Mbonde akidai kuwa hawahitaji kuongozwa tena na mwenyekiti huyo.


"Sisi wananchi hatutaki kumuona huyu mwenyekiti hata kusogelea ofisi, kwani amekuwa akikusanya ushuru wa mazao, asilimia 10 ya mauziano ya ardhi  na nyinginezo lakini mhasibu amekuwa hakabidhiwi pesa hizo matokeo yake zinapohitajika fedha za kufanya maendeleo ya kijiji huwa anasema ofisi haina fedha na tunapofuatilia tunakuta ni kweli ofisi haina fedha"


Diwani wa Kata hiyo Atanas Haule pamoja na mtendaji wa kata Yusuph Lukuwi wamethibitisha uwepo wa tuhuma hizo kwa mwenyekiti huyo pamoja na kufungwa kwa ofisi ya kijiji.


kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho Thomas Mkinga alipoulizwa juu ya tuhuma hizo zinazomkabili hakutaka kuzungumza chochote akidai mpaka atakapopata kibali kutoka ngazi za juu.


Naye mkuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amesema wanafanya uchunguzi wa karibu juu ya jambo hilo sambamba na kusuluhisha mgogoro huo ili wananchi waendelee kupata huduma kupitia ofisi hizo za kijiji.


"Niwaase viongozi wa ngazi zote kuepuka migogoro na wananchi na zinapo tokea kesi mbalimbali watatue  kwa wakati  ili kutoathiri utendaji kazi na utoaji wa huduma kwani ushirikiano ndio msingi imara katika utendaji kazi"

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post