DKT.MPANGO AZINDUA MAONYESHO YA BIDHAA ZA JKT DODOMA

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipokea zawadi ya tuzo kutoka kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa mara baada ya Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT iliofanyika mkoani Dodoma leo tarehe 01 Julai 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipanda mti aina ya Mstafeli katika eneo la Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Chamwino mkoani Dodoma wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT. Tarehe 01 Julai 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati wa Ufunguzi wa Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT mkoani Dodoma leo tarehe 01 Julai 2023. (Wengine katika Picha ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Mhe. Vita Kawawa)


Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog, DODOMA 

 JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limeadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963 na kuzindua maonyesho ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na jeshi hilo na kuahidi kuongeza ari ya kuwafundisha Vijana matumizi ya  Teknolojia kwenye uzalishaji wa chakula kuendana na wakati.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango ameshuhudia maadhimisho hayo na kufurahishwa namna Jeshi hilo linavyofanya kazi huku akitoa rai kwa wananchi kujitokeza katika wiki nzima ya maadhimisho ya miaka 60 ya JKT ili kujionea bidhaa zinazozalishwa  na kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na utengenezaji bidhaa.

Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kuliagiza Jeshi hilo(JKT )kuongeza ari ya kuwafundisha Vijana matumizi ya  Teknolojia kwenye uzalishaji wa chakula ili nchi iweze kuwa Ghala la Chakula kwa ukanda wa Afrika .

Akizungumza  leo July 1,2023 Jijini Dodoma wakati kwenye maadhimisho hayo Dkt.Mpango amesema ulimwengu wa sasa ni wa Sayansi na teknolojia hivyo ni vyema kwa Jeshi hilo kutumia teknolojia za kisasa kufundisha vijana katika kuzalisha mali zitakazokidhi ubora wa hali ya juu.

"Ninaomba Jeshi hilo lione umuhimu wa kuwatambua wataalam wake wabunifu na kuwapa tuzo sambamba na kushirikiana na Taasisi husika kuwa na haki miliki ya ubunifu na gunduzi mbalimbali zinazofanywa jeshini,"amesema.
 
Katika kutekeleza dhima ya kuwaandaa vijana wa Tanzania,Dkt.Mpango amesema JKT linapaswa kuendeleza uzalendo wa kuwajengea nidhamu, ukakamavu na kujituma ili waweze kuchangia katika ulinzi wa Taifa na maendeleo ya kiuchumi,.

Kuhusu utunzaji wa mazingira, Dkt.Mpango amelitaka Jeshi la JKT kuendeleza juhudi zake katika utunzaji wa vyanzo vya maji na kueleza kuwa anafahamu kuwa jeshi hilo ni kinara katika utunzaji wa mazingira.

Amesema,"Juhudi za kupanda miti na uhifadhi wa mazingira zifanywe na Kambi zote za JKT nchini, ili kuhakisha mazingira yanatunzwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho, namsisitiza pia matumizi ya nishati safi ili kupunguza ukataji miti ovyo,"amesisitiza

Aidha amelitaka Jeshi hilo kuunga mkono udhibiti wa taka za plastiki, kwani huchangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa mazingira na kutoa wito kwa JKT kuhakikisha wanashirikiana na Taasisi zingine katika kutafuta suluhisho la upatikanaji wa chakula cha samaki hapa nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema Wizara yake itaendelea kuijengea  uwezo JKT  ili  kuongeza uzalishaji kupitia Suma JKT na kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati.

 Amesema kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta wanatarajia kuboresha mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana wa JKT na kuwawezesha kuwapatia ujuzi na maarifa zaidi ili baada ya kuhitimu waweze kujitegemea kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali.
 
Waziri Bashungwa ameongeza,"Pamoja na malezi kwa vijana JKT tunapaswa kuwa na ubunifu na kutoa mchango kwa taifa, kuzalisha ajira na kulisaidia taifa kuwa na chakula toshelevu,lakini yote haya yanapatikana Kwa sisi kuendelea kuwa kitovu cha amani,"amesema
 
Naye  Mkuu wa Jeshi hilo Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema licha ya changamoto mbalimbali,JKT limefanikiwa kufikia dhumuni la kuanzishwa kwake kwa kutoa mafunzo ya malezi kwa vijana ili kuwajengea uzalendo, kujitegemea na kuleta maendeleo endelevu na utangamano wa kitaifa. 

"Malengo haya yametekelezwa kwa ufanisi na kufanikiwa kuwabadili vijana wetu  kifikra na kuwajenga katika hali ya umoja, moyo wa kupenda kazi, uadilifu, nidhamu, uzalendo na uelewano bila kubaguana kwa misingi ya ukabila, udini, jinsia na kudumisha uhuru na amani ya Taifa,"amefafanua Mkuu huyo wa JKT na kuongeza;
 
"Naishukuru sana Serikali kwa kuendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto za Jeshi letu ikiwemo kuendelea kutenga fedha ili kuboresha miundombinu itakayowezesha kuchukua vijana wengi zaidi kwa ajili ya mafunzo,ni matumaini yangu kwa kila mtanzania kuendeleza uzalendo wa kujituma na kujifunza mengi kupitia JKT,"amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post