WATOTO WAWILI WAFARIKI KWA KUUNGUA MOTO NDANI YA NYUMBAMkuu wa wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga

Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Watoto wawili wa familia moja katika Kitongoji cha Kyajoshwa Kijiji cha Kanyamika Wilayani Muleba Mkoani Kagera wamekutwa  wamefariki kwa kuungua na moto wakiwa ndani baada ya nyumba yao kuungua moto na chanzo cha tukio kikiwa hakijatambulika.


Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kyajoshwa Bwana John Bakilana amewataja watoto hao kuwa ni Mariam Mateso mwenye umri wa miaka miwili na Laulent Mateso mwenye umri wa miaka mitatu na kwamba tukio hilo limetokea Julai 2,2023 majira ya jioni wakati baba yao mzazi akiwa mtoni anateka maji.

Bwana Bakilana amesema kuwa tukio hilo ni la  pili ndani ya familia hiyo ambapo tukio la kwanza lilitokea Juni 28 mwaka huu wakiwa ndani wamelala lakini walitoka wakiwa salama ndipo likatokea tukio hilo na kuua watoto hao ambapo chanzo chake hakijajulikana.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dkt. Abel Nyamahanga ameagiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina na kwa wakati kujua chanzo cha tukio hilo huku akiwataka wananchi kuwa na subra na kutojichukulia sheria mkononi kwa kutuhumu mtu ambaye hana hatia na kusababisha uvunjifu wa amani.

Aidha jeshi la polisi Wilayani humo limefika eneo la tukio na kuruhusu taratibu za mazishi ziendelee.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post