CCM: UWEKEZAJI BANDARI DAR HATUTARUDI NYUMA, SERIKALI ONGEZENI KASI KUKAMILISHA MCHAKATO


Na Mwandishi Wetu-Michuzi TV- Mtwara

CHAMA Cha Mapinduzi( CCM) kimeitaka na kuisisitiza Serikali kuhakikisha inaharakisha mchakato wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam na kwenye hilo Chama hicho hakitarudi nyuma na wala hakitayumbishwa na wanaopinga uwekezaji huo.

Akizungumza katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kwenye mkutano mkubwa wa hadhara, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Daniel Chongolo amesema wanaohoji kuhusu uwekezaji huo wanajua wakiacha ikatekeleza yote kwa ufanisi kazi yao ni ngumu huko mbele ndio maana wanahaingika kukwamisha

"Sasa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ukiangalia ibara ya 22 inaeleza namna mipango ya uwekezaji ikiwemo bandari ilivyondikwa na kuainishwa wazi lakini ukienda kwenye ibara ya 59 ukurasa wa 92 wa Ilani yetu imeweka wazi kwa kuanisha namna mipango ya uwekezaji ilivyo kwenye bandari nchini.

"Leo wanaamisha ajenda hawataki kujadili Ilani ya uchaguzi na kwamba huu ni utekelezaji wa Ilani ili ninyi mbakie mkifikiri linalotekelezwa sio la kwenu , hili linalotekelezwa ni la CCM, ni ahadi ya CCM na tunatekeleza wana CCM...

"Kwasababu ndio tumepewa dhamana ya kuongoza nchi na hatuna mahali pengine , hatuna msalia mtume , hatuna hofu , hatuna mashaka hili jambo tutalitekeleza kwasababu ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi. Wanaohangaika kuibadilisha na kuifanya iwe ya Rais wamekosea muelekeo wa kulifanya liende huko wanakotaka.

"Tumewagundua, tunawajua , tunajua njia wanazotumia na ndio maana tunaitwa Chama tawala nchini , tunaona kuna watu wamekaa kienyeji, wajifunze kwamba kuongoza nchi sio kazi lelemama , kupepeta mdomo ni kazi rahisi kutenda ni kazi ngumu, " amesema Chongolo.

Amesisitiza ushabiki, uzushi ni kazi rahisi lakini kazi ya kutenda ni kazi ngumu haina msalia mtume haina lele mama na kwamba yeye Katibu Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Chama hicho toka jana na leo anarudia tena kuitaka Serikali iongeze kasi kwenye mchakato ili wafike mwisho na kupata matokeo yake na sio vinginevyo .

"Ukimuona adui yako anakupigia makofi unapofanya jambo achana nalo haraka kimbia tengeneza mkakati mpya wa kulitenda lakini ukimuona amenuna , anahangaika anapambana lisifanikiwe nyoosha mguu kanyaga mwendo hiyo ndio kwako faida.

" Na hili ninyi ni mashahidi angalieni sura zao, matamanio yao wote hawataki litokee , niwahakikishie litatokea tuko salama na tutafikia malengo na ndio kazi ya Chama kinachojitambua , chama chenye wajibu .Ni wahakikishie mambo yakitokea mapato yakiongezeka tunashindwaje kuongeza hata Newala kukawa na uwanja wa ndege mkubwa wa kisasa.

"Suala ni uwezo, ni wahakikishie na nisisitize tuko imara, tuko timamu wala hatuna habari ya kutumia muda mwingi , najua wana CCM mnajitambua mnajua dhamana yenu na wajibu wa kuisimamia Serikali itekeleze Ilani inavyotakiwa , tusome, tuelimishe wenzetu tusimamie hapo hapo, " amesema Chongolo.






















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post