TUTASHIRIKIANA NA WOTE WENYE NIA YA KUTOKOMEZA UKATILI - WAZIRI DKT. GWAJIMAWaziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa kata ya Ihumwa kuhusu Kampeni ya ONGEA NAO aliyoizindua katika kata hiyo Juni 3, 2023 kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi pamoja na Kituo cha Redio cha Afm.


Diwani wa kata ya Ihumwa Mhe. Edward Magawa akizungumza wakati wa tukio la uzinduzi wa Kampeni ya "ONGEA NAO" iliyozinduliwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dorothy Gwajima, Juni 3, 2023 jijini Dodoma kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na kituo cha Redio cha Afm.


Naibu Kamishna wa Polisi Maria Nzuki kutoka Kamisheni ya Jinsia akieleza lengo la Kampeni ya "ONGEA NAO" iliyozinduliwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dorothy Gwajima, Juni 3, 2023 jijini Dodoma kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na kituo cha Redio cha Afm.


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kampeni ya ONGEA NAO inayofanywa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na kituo cha redio cha Afm cha jijini Dodoma, Juni 3, 2023.


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akichanganya udongo wakati akishuhudia ujenzi wa kituo cha Polisi cha kata ya Ihumwa amnavho kitasaidia kudhibiti uhalifu ikiwemo vitendo vya ukatili, baada ya uzinduzi wa Kampeni ya "ONGEA NAO" inayofanywa na Jeshi la Polisi kwa ushirikiano na kituo cha redio cha Afm, Juni 3, 2023.


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima katika picha ya pamoja na Maafisa wa Jeshi la Polisi walioshiriki uzinduzi wa Kampeni ya "ONGEA NAO" inayofanywa na Jeshi hilo kupitia Kamisheni ya Jinsia kwa ushirikiano na kituo cha redio cha Afm, Juni 3, 2023.

Na WMJJWM, Dodoma

Serikali imesema itashirikiana na wananchi pamoja na wadau wote walio tayari kutokomeza vitendo vya ukatili ndani ya Jamii.

Kauli hiyo Imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizindua Kampeni ya "ONGEA NAO" iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi jijini Dodoma kwa kushirikiana na kituo cha redio cha AfM cha jijini Dodoma, Juni 03, 2023.

Mhe. Gwajima amesema pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kuhimiza maadili mema na Upendo ndani ya jamii, bado kuna matukio mengi ya ukatili wa kijinsia katika familia na wahanga wakubwa ni wanawake na watoto.

"Kwa mujibu wa taarifa ya makosa ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kutoka Jeshi la Polisi kwa Januari hadi Disemba 2022, jumla ya matukio ya ukatili kwa watoto yalikuwa 12,163 (wavulana 2,201 na wasichana 9,962) ukilinganisha na matukio 11,499 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la matukio 664" amesema Dkt. Gwajima.

Ameongeza kuwa, ukatili wa kijinsia huchangiwa na kuporomoka kwa maadili na changamoto za kiuchumi ndani ya familia ambapo madhara mojawapo ni kupunguza nguvu kazi ya taifa, kuleta umasikini katika familia na kusababisha jamii kuishi kwa hofu hivyo ana imani baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo jamii itapata elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua ya kupunguza matukio ya ukatili.

Wakati huo huo Mhe. Gwajima ametoa rai kwa Wazazi na Walezi kuhakikisha wanawalinda na kuwathamini watoto, kuwa wepesi kutoa taarifa inapotokea au wanapokutana na vitendo vya ukatili wa kijinsia huku akiziasa baadhi ya jamii zinazoendeleza mila na desturi zenye madhara kwa jamii ukatili wa kijinsia kuacha.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Polisi Maria Nzuki kutoka Kamisheni ya Jinsia amesema Kampeni hiyo inalenga kuisogeza jamii karibu na jeshi la Polisi ili kujenga uelewa wa kujua viashiria vya ukatili kabla haujatokea.

"Mradi huu utagusa maeneo mbalimbali nchini kwa kuanza na mkoa wa Dodoma. Uzinduzi huu ni mwanzo wa uzinduzi ndani ya mikoa yote nchini." amesema Maria Nzuki.

Naye Diwani wa kata ya Ihumwa ilipozinduliwa kampeni hiyo, Mhe. Edward Magawa amebainisha kwamba kampeni hiyo imekuja wakati muafaka ambapo kata hiyo ina miradi mingi ya Serikali, hivyo wageni ni wengi wakiwemo wahalifu.

"Kata yetu tumeamua kupinga vitendo vya ukatili kwa vitendo, ili kuliongezea nguvu jeshi la polisi, tumeamua kujenga kituo cha polisi cha kata ya Ihumwa." amesema Mhe. Edward.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post