BALOZI CHEN MINGJIAN ATEMBELEA MRADI WA UPANUZI WA KUZALISHA MAJI WAMI


BALOZI wa China nchini Tanzania Mhe.Chen Mingjian amefanya ziara kutembelea na kukagua Maendeleo ya Utekelezaji wa Mradi wa upanuzi wa Mtambo wa kuzalisha Maji Wami ambapo ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wasimamizi wa mradi huo DAWASA.

Akizungumza katika ziara hiyo leo Juni 26,2023 amesema Serikali ya China iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha miundombinu ya kuzalisha maji kwenye mtambo wa Wami ili uweze kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Aidha amesema wataendelea kishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mikakati ya uboreshaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira

"Tunaipongeza DAWASA kwa hatua ilizozichukua za kuboresha miundombinu pamoja na kufanya upanuzi wa mtambo, hizi ni jitihada kubwa za kupongezwa, kwa kuwa zinalenga kutoa huduma kwa wananchi wengi," amesema Balozi Chen.


Nae Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Bw. Kiula Kingu amesema kuwa ziara ya Mhe. Balozi imelenga kufuatilia maendeleo ya mtambo huo tangu ulipojengwa mwaka 2001 kwa ufadhili wa Serikali ya China.

Amesema kuwa nia haswa ni kuangalia mitambo yote na mifumo yote iliyopo ili kubaini ni sehemu gani wanaweza kuboresha na kuongeza nguvu kwa lengo la kukuza uzalishaji wa maji na kukidhi mahitaji ya wananchi wa maeneo haya.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Exim India, imefanya maboresho ya upanuzi wa uzalishaji wa mtambo wa maji kutoka lita milioni 7.2 mpaka lita milioni 21 kwa sasa na kuweza kuhudumia wananchi 197,000 na vijiji 47.

"Mpaka sasa utekelezaji wa mradi wa Chalinze awamu ya tatu umefikia asilimia 95" alisema na kuongeza kuwa kazi iliyobaki ni kuweka mifumo ya tehama ili kuweza kusimamia miundombinu ya mradi huu wenye kugusa mikoa ya Pwani na maeneo ya mikoa ya Morogoro na Tanga.

"Mifumo hii itaiwezesha DAWASA kufuatilia mwenendo wa ujazaji maji katika matenki na usambazaji maji," ameeleza Ndugu Kingu.

"Lengo la maboresho haya ni kuhakikisha tunakuza upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya mijini na vijijini yanayohudumiwa na mradi huu kwa asilimia 95 mijini na 85 vijijini," ameongeza.

Kwa upande wake Bi Mwajuma Saidi mkazi wa Msata ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuwatua ndoo kichwani wakazi wote wa eneo lao.

"Kero ya maji ilikuwa kubwa kwenye eneo hili, tulikuwa tunafuata maji bondeni yenye chumvi ambayo hayakuwa salama kiafya, kwa sasa tunashukuru shida imeisha," ameeleza.

Mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu umetekelezwa na DAWASA kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi 274,603 wa mji wa Chalinze, Morogoro, Pwani, Ngerengere na baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post