RAIS  DKT. SAMIA AMWAPISHA JAJI (Mst.) TEEMBA KUWA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAADILIRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, (Kushoto) akimwapisha Mhe. Jaji (Mst.) Rose Teemba (Mwenye suti ya kijivu) kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma tarehe 23.5.2023.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi,(hayuko pichani) akiongoza kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa waheshimiwa majaji wa Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Maadili katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu chamwino, jijini Dodoma tarehe 23. 5.2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,(wa pili kushoto), Mhe. Kassim Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (wa kwanza kushoto), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri (wa tatu kushoto) na Jaji. Sivangilwa Mwangesi, Kamishna wa Maadili wakiwa katika picha ya pamoja na waheshimiwa majaji wa Rufani, Mwenyekiti wa Baraza la Maadili na watendaji wa Wizara ya Katiba na Sheria Ikulu, Chamwino jijini Dodoma tarehe 23.5.2023.

Na.Mwandishi Wetu-DODOMA

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemwapisha Jaji (Mst.) Rose Teemba kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino jijini Dodoma tarehe 23.5.2023.

Mhe. Rais alimteua Jaji Teemba tangu tarehe 24.4.2023 kwa mujibu wa kifungu cha 26(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 kinachoeleza kuwa Baraza la Maadili litakuwa na wajumbe watatu watakaoteuliwa na Rais, miongoni mwao akiwemo aliyeteuliwa kutoka miongoni mwa watu wenye wadhifa au wamewahi kuwa na wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu.

Aidha, kifungu hicho cha 26(3) kinasema kuwa Rais, atateua mmojawapo wa Wajumbe wa Baraza kuwa Mwenyekiti.

Katika hafla hiyo, Mhe. Rais ameeleza kuwa hana mashaka na uzoefu katika utendaji kazi wa Jaji Teemba.

“Jaji Sivangilwa Mwangesi, Kamishna wa Maadili akisha maliza kazi yake anakuleteeni nyinyi Baraza la maadili, ichambueni vizuri na kutuletea mapendekezo yenu,” amesema na kuongeza kuwa, “Tuna matatizo makubwa kwenyey eneo la uadilifu katika utawala, shughulikieni.”

Kazi kubwa ya Baraza la Maadili ni kufanya uchunguzi wa kina wa malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya viongozi wa umma waliotajwa katika kifungu cha 4 cha Sheria hiyo.

Aidha, uchunguzi huo hutanguliwa na uchunguzi wa awali ambao kwa mujibu wa kifungu cha 18(2)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, hufanywa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Jaji mstaafu Teemba anachukua nafasi ya Jaji mstaafu Ibrahim Mipawa aliyemaliza muda wake, akiongoza Baraza hilo tangu Agosti 16, 2019 alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Jaji mstaafu Teemba anakuwa Mwenyekiti wa tano wa Baraza la Maadili toka kuanzishwa kwake akitanguliwa na Jaji mstaafu Damian Lubuva, Jaji mstaafu Hamis Msumi, Jaji mstaafu Januari Msofe na Jaji mstaafu Ibrahim Mipawa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post