Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amekabidhi Pikipiki Nane kwenye Kata zote nane za Halmashauri ya Mji Kondoa Mkoani Dodoma zenye thamani ya Shilingi Milioni 21 kwa ajili ya kusaidia Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Chama Cha Mapinduzi kwenye Kata hizo.
Mbunge Ditopile amekabidhi Pikipiki hizo wakati wa kuhitimisha ziara ya siku nne ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kondoa, Hija Suru ya kuwashukuru wanachama kwa kumchagua kuongoza chama hicho ngazi ya Wilaya.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vitendea kazi hivyo pamoja na vifaa vingine, Mbunge Ditopile amesema ataendelea na jitihada za kuhakikisha anarahisisha utendaji kazi wa viongozi wa chama ili kuongeza chachu ya kusimamia miradi ya Serikali inayotekelezwa kwenye maeneo yao sambamba na kurahisisha shughuli za uendeshaji na uimarishaji wa chama ndani ya Wilaya hiyo.
"Kama chama tuna kazi kubwa ya kumsaidia Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan katika kusimamia miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa kwenye maeneo yetu, Mhe Rais na Serikali yake wanafanya kazi kubwa ya kuleta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali, ni jukumu letu sisi wasaidizi wake huku chini kuhakikisha tunamsaidia kuisimamia.
"Nimekabidhi Pikipiki hizi nane ambazo naamini zitakua na mchango mkubwa kwa Mwenyekiti na Katibu wa Chama kwenye Kata zetu zote za Kondoa Mjini katika kukiimarisha chama lakini pia kusimamia utekelezaji wa ilani ya Chama chetu"
"Mwaka 2025 tunalo jukumu la kuhakikisha tunamvusha Rais wetu wa kwanza mwanamke, Dkt. Samia Hassan, na kwa kazi kubwa ambayo anafanya katika kuwatumikia watanzania basi ni deni kwetu wasaidizi wake kufanya kazi huku chini ya kumsaidia na kuwatumikia wananchi waliotuamini," Amesema Mbunge Ditopile.
Katika ziara hiyo pia Ditopile amechangia Shilingi Milioni 2.5 kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi katika kata za Masange, Kisese, Thawi, Migungani, Salanka, Mafayi Haubi ambazo ziko katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
"Niwaahidi kwamba niko tayari kutumwa, ndio maana niliposikia kuna mgogoro kati ya Gereza na Wananchi kule Kata ya Kingale haraka nilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni nae alifika na kutusikiliza na ameahidi Disemba 30 majibu yatapatikana, hii inaonesha pia jinsi gani Serikali yetu ya awamu ya sita inawajali wananchi wake," Amesema Mbunge Ditopile.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kondoa, Hija Suru amemshukuru Mbunge Mariam Ditopile kwa mchango wake wa kukiimarisha chama huku akiwataka viongozi waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitunza na kuzitumia katika kuwatumikia wananchi na kukiimarisha Chama kwenye maeneo yao.