KAMATI YA BUNGE YA BAJETI YAKAGUA SHUGHULI ZA UPAKUAJI NA UPIMAJI MAFUTA DAR ES SALAAM

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika eneo la gati ya kushushia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam mara baada ya kufika bandarini hapo kuona jinsi shughuli za ushushaji na upimaji mafuta zinavyofanyikaMwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo akizungumza jambo wakati Kamati hiyo ikiwa katika sehemu ambayo inaruhusu mafuta kutoka kwenye meli kwenda kwenye sehemu za kuhifadhia mafuta zinazomilikiwa na kampuni mbalimbali zinazofanya biashara ya mafutaWajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika eneo la kupima mafuta katika eneo la Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Baadhi ya miundombinu iliyopo katika eneo lililofungwa mita za kupimia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.

.........................

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imefanya ziara katika maeneo yanayotumika kupakua mafuta kutoka kwenye Meli na kupima katika Bandari ya Dar es Salaam na Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Ziara hiyo ilifanyika tarehe 13 Oktoba, 2022 ikiwa na lengo la kujihakikishia kuwa kazi za ushushaji wa mafuta na upimaji mafuta katika sehemu hizo zinafanyika kwa ufanisi na Serikali inapata mapato stahiki.

Baada ya kufanya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mhe.Daniel Sillo, aliipongeza Serikali kwa jinsi ilivyowekeza katika miundombinu ya ushushaji wa mafuta pamoja na mita za kupimia mafuta hayo ambazo kwa miaka ya nyuma zilikuwa hazipo na hivyo Serikali ilikuwa haipati mapato stahiki.

Alisema kuwa, mita hizo za kupimia mafuta licha ya kuiwezesha Serikali kupata mapato inayostahili, kampuni zinazoagiza mafuta hayo kutoka nje ya nchi pia zinapata uhakika wa kiasi cha mafuta ambacho wamekiagiza.

Vilevile alisema kuwa, Kamati hiyo ilifanya ziara katika Bandari ya Mtwara ambapo pia Wajumbe walishuhudia juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuiendesha sekta ya mafuta kwa ufanisi kwani mita za kupimia mafuta katika bandari hiyo zinafanya kazi vizuri na pia upanuzi wa bandari pamoja na sehemu za kuhifadhia mafuta unaendelea vizuri hali itakayofanya bandari hiyo kupokea mafuta kwa wingi zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments