MWANAFUNZI DARASA LA TANO AJINYONGA BAADA YA KUMALIZA KUNYWA CHAI



Na Halima Khoya, SHINYANGA

Mwanafunzi wa darasa la tano  katika shule ya msingi Ndala ‘A’ Manispaa ya Shinyanga Brayton Daniel (11) amekutwa amejinyonga kwa kutumia kamba nyuma ya mlango nyumbani kwao.

Tukio hilo limetokea Oktoba 26 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi katika Mtaa wa Mwabundu Kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga.

Akielezea tukio hilo  mama mkubwa wa marehemu Joyce Kalulu, amesema mtoto huyo hakuwa na tatizo lolote, lakini siku hiyo walipomaliza kunywa chai, yeye alikwenda kwenye mihangaiko yake ya maisha na aliporudi nyumbani majira ya saa 8 mchana akakuta mlango umefungwa kwa ndani na walipovunja wakabaini kuwa kijana wao amejinyonga.

“Asubuhi nimeamka na kufanya kazi zote nikawa nimewaacha kijana wangu na bibi yake, nimerudi saa 8 kutoka kazini nikamkuta mama anahangaika kumuita Brayton afungue mlango, ndipo tulipoamua kwenda kumuita Mwenyekiti ambaye alifanikiwa kutoboa nyavu za dirisha na kumuona Brayton akiwa amening’inia mlangoni,”amesema Kalulu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwabundu Pili Masanja amesema taarifa za tukio hilo alizipata majira ya saa 9 mchana, na alipofika kwenye familia hiyo ikabidi watoboe nyavu ya dirisha alipochungulia akamuona mtoto huyo akiwa amejinyonga nyuma ya mlango.

“Majira ya saa 9 nilikuja kuitwa na Joyce Kalulu ili nikawasaidie kufungua mlango ambapo nilizunguka nyuma ya nyumba ili kutoboa dirisha lakini tulichokiona baada ya kutoboa dirisha ni Brayton akiwa amejinyonga na kamba nyeusi kwenye mlango, ndipo nikapiga simu Polisi,”amesema Masanja.
Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa Shinyanga Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akibainisha kuwa Jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments