MKUTANO WA WADAU KUJADILI MAPITIO YA SERA YA ELIMU NA MITAALA KUFANYIKA KWA SIKU TATU JIJINI DODOMA.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Prof Adolf Mkenda.


Na Mathias Canal, WEST-Dodoma.

Serikali imeandaa mkutano maalumu kwa mara nyingine wa wadau wa elimu kutoka maeneo na sekta mbalimbali nchini kote nchini utakaofanyika Jijini hapa kwa lengo la kuboresha elimu nchini .


Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo tarehe 25 Septemba 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 Septemba 2022 Jijini Dodoma.


Waziri Mkenda ameeleza lengo la Mkutano huo kuwa ni kujadili Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mabadiliko ya Mitaa ya Elimu msingi. 


Amesema kuwa Majadiliano hayo yatatokana na hatua iliyofikiwa na mapitio hayo kupitia kamati maalumu zilizopewa majukumu hayo.


Waziri Mkenda amesema kuwa Mkutano  huo unajumuisha, Wahadhiri, Waajiri, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za umma na Binafsi, Taasisi za Dini, Taasisi zinahusika na uendelezaji wa lugha, Wabunge, Wajumbe toka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Taasisi zisizo za Kiserikali, Jumuiya za kitaaluma, na Taasisi za Sayansi na Utafiti.


Katika hatua nyingine, Waziri Prof Mkenda amesema kuwa tarehe 27 Septemba, 2022 serikali itatangaza rasmi majina ya wanafunzi waliopata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIPS”. 


"Mtakumbuka Wizara yetu ilitoa ahadi kupitia hotuba ya bajeti ya kuanzisha programu mpya ya kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wahitimu bora wa kidato cha sita katika masomo ya sayansi. Hivyo mpaka sasa tuna majina karibu 600 ya wanafunzi ambao wamechaguliwa" Amekaririwa Waziri Mkenda


Kadhalika, Waziri Mkenda ameukumbusha umma kuwa serikali imezindua tuzo za waandishi bunifu zijulikanazo kama Tuzo za Mwalimu Nyerere, hivyo ameendelea kukaribisha Waandishi Bunifu wa Riwaya na Mashairi kuwasilisha maandiko yao ili kuwania tuzo hizo. 


Prof Mkenda amesema kuwa Mwisho wa kupokea Mawasilisho hayo ni  Novemba 30, 2022 ambapo kwa taarifa zaidi kuhusu tuzo hizo na maulizo wanaweza kufuatilia katika akaunti maalumu za mitandao ya kijamii za  tuzo Nyerere au mitandao na tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Elimu Tanzania-TET kwa anuani ya tuzonyerere@tie.go.tz
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post