TAKUKURU YAWATAKA WANAFUNZI KUVUNJA UKIMYA RUSHWA YA NGONO CHUONI


Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Bw. Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 10,2022
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Bw. Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 10,2022
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Bw. Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 10,2022

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imewataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na vyuo vya kati kuvunja ukimya kwa kutoa taarifa kuhusu rushwa ya ngono inayofanywa na Wahadhiri na Wakufunzi.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Bw. Donasian Kessy leo Jumatano Agosti 10,2022 wakati akitoa taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Aprili – Juni,2022).

Kessy amesema kumekuwa na viashiri kwenye vyuo vya elimu ya juu na vyuo vya kati kwamba Wanafunzi hususani wa kike wamekuwa wakitishiwa kufelishwa kwenye mitihani yao na wahadhiri wao hivyo kuombwa rushwa ya ngono na walimu hao ili wawapendelee kwenye mitihani yao.

"Kuna viashiria vya rushwa ya ngono wahadhiri wana tabia ya kutaka rushwa ya ngono ili wawapendelee kwenye mitihani na wanatumia mbinu mbalimbali za kuwafelisha kwenye mitihani. Tumebaini hili tatizo lipo lakini wanafunzi hawatoi taarifa",amesema.

“Wanafunzi vyuoni vunjeni ukimya kuhusu rushwa ya ngono. TAKUKURU inaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya rushwa. Tumekuwa tukitoa rai Vyuo vinapofunguliwa, Wanapoingia wanafunzi wapya kwenye  wiki ya kwanza tuje tutoe elimu ya masuala ya rushwa ili kudhibiti rushwa ya ngono chuoni. Naomba mtuite tuje kutoa elimu ili wanafunzi wapya wajue wapi pa kupeleka taarifa wanapokutana na matukio haya ya rushwa ya ngono. Tunaomba watoe taarifa  tufuatilie ili hatua za kisheria zichukuliwe",amesema Kessy.

Amesema TAKUKURU inaendelea na kampeni ya VUNJA UKIMYA KATAA RUSHWA YA NGONO kwenye vyuo mbalimbali. Katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2022 Kampeni hii imefanikiwa kuelimisha vijana takribani 541 wa Chuo cha VETA, Chuo cha Ushirika Tawi la Kizumbi Shinyanga (MoCU) na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Buhangija ambapo wito wa Vunja Ukimya :Kataa Rushwa ya Ngono ulitolewa.

“Pia tumetembelea kuimarisha Klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi na sekondari ambapo tumetembelea Klabu 35 za wapinga rushwa ambapo takribani wanafunzi 1525 walielimishwa juu ya umuhimu wa kushiriki mapambano dhidi ya rushwa. Tunashukuru kumekuwa na mwamko mkubwa wa vijana kushiriki mapambano haya”,ameeleza.


Ameeleza kuwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga inaendelea na kampeni maalumu ya TAKUKURU INAYOTEMBEA kuwafuata wananchi katika mikusanyiko na kuwaelimisha kwa kutumia vipaza sauti namna ya kutoa taarifa za vitendo vya rushwa huku wakiendelea na shughuli zao za kujipatia kipato.


Kessy amewataka wananchi wa mkoa wa Shinyanga kutoa ushirikiano kwa serikali yao,kuhakikisha miradi yote inayoendelea inakamilika kwa ubora na kama wataona kuna vitendo vyovyote ambavyo vinaashiria ubadhirifu wa miradi watoe taarifa TAKUKURU.

“TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga inatoa wito kwa wananchi wanapoona kuna vitendo vyovyote vya rsuhwa kutoa taarifa katika ofisi za TAKUKURU kwa kufika ofisi zetu zilizopo Shinyanga au wapige simu namba 0738 150196 au 0738150197, Ofisi ya Kahama 0738150198 na Ofisi ya Kishapu 0738150199”,ameongeza Kessy.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post